Ticker

6/recent/ticker-posts

NICOL YAPELEKA NEEMA KWA WANAHISA WAKE SABASABA

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Uwekezaji ya NICOL, imeendelea kufanya vizuri sokoni kwa kupata ongezeko ya faida ya shilingili bilioni 6.2 mwaka huu kulinganisha na faida ya shilingi bilioni 4.1 ya mwaka 2021.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NICOL, Erasto Ngamilaga, wakati akizungumza na gazeti hili kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya sabasaba vya Mwalimu Julius Nyerere.

“Faida hiyo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 51 na mapato ya kila hisa nayo yameongezeka kwa asilimia 42 kwa hiyo haya ni mapinduzi makubwa sana kwenye kampuni yetu na wanahisa waendelee kutarajia maakubwa zaidi kwa mwaka 2023,” alisema

Aidha, Erasto alisema viongozi wa kampuni hiyo wameendelea kuwa na maono na mikakati madhubuti inayoenda sambamba na uwekezaji wenye lengo la kuongeza mapato ya wanahisa wake.

Erasto alisema takwimu za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zinaonyesha kuwa Kampuni ya NICOL inaendelea kufanya vziuri kwani hisa zake kwa sasa zinauzwa kwa Shilingi 475 kwa hisa moja.

“Mwelekeo ni mzuri sana na kwa tunavyokwenda muda si mrefu hisa zetu zitaanza kuuzwa kwa shilingi 1,000 ndiyo maana tunawashauri wananchi wachangamkie hisa zetu kwani zinafaida kubwa,” alisema

Aidha, alisema kupanda kwa thamani ya hisa za kampuni hiyo kunatokana na jitihada za manejimenti ya kampuni hiyo kuongeza mapato kwa wanahisa kwa kufanya utawanyaji wa uwekezaji kwenye maeneo yenye faida.

“Kwa sasa uwekezaji wa Kampuni yetu umefikia shilingi bilioni 130 na tumeamua kuja hapa kwenye maonyesho ya sabasaba kuwapa fursa wanachama ambao hawakupata fursa ya kufika ofisini kwetu na kuchukua gawio lao kwa miaka mingi waje hapa watapata huduma nzuri sana,” alisema Erasto

Alisema tangu kampuni hiyo ilipoanza kutoa gawio mwaka 2017 ni miaka sita sasa kuna wanahisa ambao hawajapata gawio lao hivyo kuwepo kwao saba saba ni kujaribu kuwarahisishia wanahisa hao kwenda kujaza fomu ili walipwe gawio lao.

“Kupitia maonyesho haya tunaimani tutaongeza idadi ya wanahisa ambao wanataka kuwekeza NICOL na wale ambao walikuwa wamekata tamaa tunawaambia tupo vizuri sokoni na tunamikakati mikubwa ya siku za baadae,” alisema

Alisema wananchi ambao bado hawajawekeza wachangamkie fursa hiyo na kuwekeza kwani mikakati ya kampuni hiyo kwa sasa itaiwezesha kampuni kupata faida na kutoa gawio nono kwa wanachama wake kila mwaka na kuwashauri wananchi kufika ukumbi wa Karume sabasaba ambapo watahudumiwa kama ofisini.

Aidha, alisema wanaendelea kuwa na mikakati ya upanuzi wa uwekezaji ambapo sasa wanangalia maeneo yenye tija ambayo yatawaongezea kipato wanahisa wa NICOL na kuchangia kwenye jitihada za serikali za kukuza na kustawisha uchumi wa nchi.

Alisema kwa sasa Kampuni ya NICOL inaangalia uwekezaji kwenye biashara ya gesi na shughuli za kilimo ambapo wataangalia uanzishaji wa maghala mbalimbali ya mazao ya kilimo na maeneo mahsusi ya uwekezaji kwenye maeneo ya madini.

“Tunawaomba wananchi ambao wanataka kununua hisa zetu wawasiliane na mawakala wa Soko la Hisa DSE ambao wako wengi Dar es Salaam na unaweza kuwapata kupitia namba zilizoko kwenye tovuti ya DSE,” alisema.


Ofisa Uhusiano wa wanahisa wa Kampuni ya Uwekezaji ya NICOL, Irene Nkya, (kushoto) akiwahudumia baadhi ya wateja waliofika kwenye banda lao jana kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uwekezaji NICOL, Erasto Ngamilaga

Post a Comment

0 Comments