Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS DKT.MWINYI AZUNGUMZA NA UJUMBE WA UNESCO IKULU ZANZIBAR.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa UNESCO ukiongozwa na Prof. Georg Abungu na ujumbe wake (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 20-7-2023 na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na mgeni wake Kiongozi wa Ujumbe wa UNESCO Prof. Georg Abungu, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 20-7-2023.(Picha na Ikulu)

********************

Zanzibar,

20 Julai, 2023,

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kujadili masuala mbalimbali kuhusu utunzwaji wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe.

Dk. Mwinyi alikutana na ujumbe huo Ikulu, Zanzibar ukiambata na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohammed Said pamoja na maafisa wa Wizara hiyo.

Alisema, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Zanzibar bado Urithi wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe unaendelea kulindwa na kuenziwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizowekwa.

Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe huo kwamba, Selikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali za kuutunza urithi ikiwemo kuondosha msongamano wa maegesho ya vyombo vya moto kwenye maeneo yote ya Mji Mkonge wa Zanzibar, ili kuenzi haiba ya mji huo kuendelea kuwa kivutio mashuhuri cha watalii na wageni wanaoutembelea mji huo.

Aidha, alisema katika kutekeleza hatua hiyo, Serikali imeamua kujenga maegesho ya vyombo vya moto eneo la Darajani ikiwa njia mbadala ya kuondosha msongamano wa magari kwenye maegesho ya Mji Mkongwe.

Pia Dk. Mwinyi, aliueleza Ujumbe huo kwamba hatua nyengine iliyochukuliwa na Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi kuutunza Urithi huo hasa kuyaendeleza majengo yaliyochakaa kwa kuyakarabati kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kuyaenzi majengo hayo kuyarudisha kwenye uhalisia wake.

Alisema, Serikali inasimamia kwa karibu na kuhakikisha thamani na mali zote za asili zilizokuwemo kwenye majengo hayo zinarudishwa sehemu husika baada ya ukarabati.

Akizungumzia jengo la Beit el Ajaaib na la People’s Palace, Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe wa UNESCO kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Oman wanaendelea kusimamia ujenzi wa majengo hayo.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi alieleza Beit el Ajaaib na la People’s Palace ni alama muhimu inayoitambulisha Zanzibar duniani kote.

Nao, Ujumbe huo wa UNESCO, uliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuendelea kuuenzi na kuutunza urithi huo ili kuunusuru na athari za mabadiliko ya teknolojia ikiwemo kukua kwa maendeleo ya nyanja mbalimbali nchini ambayo kwa namna moja ama nyengine itakua sababu ya kubadili mandhari halisi na mwonekano wa mji huo.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

Post a Comment

0 Comments