Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YANUNUA MTAMBO WA KUCHORONGA JOTOARDHI

Ofisa Mkuu wa Mawasiliano Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Khadija Faru akionesha picha ya mtambo wa kuchoronga visima vya kuzalisha nishati ya Jotoardhi.

************************

Na Selemani Msuya

SERIKALI imenunua mtambo wa kisasa uligharimu zaidi shilingi bilioni 13 kwa ajili yakuchoronga visima vya uzalishaji wa nishati jadidifu ya Jotoardhi ambayo ni safi na salama kwa mazingira.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mkuu wa Mawasiliano Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TDGC), Khadija Faru wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 47 yaliyoendelea katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imedhamiria kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali, hivyo dhamira hiyo ili iweze kutimia ni lazima nishati ya umeme safi na salama iweze kuzalishwa na TGDC ni moja ya taasisi yenye jukumu hilo.

Ofisa huyo amesema mtambo huo ambao umegharibu zaidi ya shilingi bilioni 13 utafanikisha lengo la uzalishaji wa megawati 200 za nishati jadidifu ifikapo 2025.

“Mwaka huu tunashiriki maonesho ya sabasaba tukiwa na furaha na amani kwani kauli mbiu ya maonesho ya ‘Tanzania Mahali Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji’ tunaenda kuitekeleza kivitendo sisi kama TGDC kupitia mtambo huu mpya ambao Serikali imenunua,” amesema.

Faru amesema kwa kuanzia mtambo huo wa kisasa utawezesha uzalishaji wa megawati 200 katika visima vitano vya Kiejombaka, Songwe, Ngozi, Ruhoi na Natroni.

Ofisa huyo amesema nishati hiyo ya jotoardhi ni ya uhakika na endelevu, hivyo ni imani yao kupitia mtambo huo wa kuchoronga watafanikiwa kuchimba katika maeneo yote ambayo yatabainika kuwa na nishati hiyo.

Amesema faida nyingine ya nishati ya jotoardhi ni pamoja na kukausha mazo, kufuga na tiba ya magonjwa mbalimbali, hivyo amewaomba wawekezaji kuja kuwekeza katika eneo hilo.

Faru amesema TGDC itahakikisha inatumia mtambo huo kufanikisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kuwapatia Watanzania nishati endelevu safi na salama.

“Tunawaomba Watanzania kutembelea banda letu lilipo sabasaba ili waweze kupata taarifa za fursa zilizopo katika nishati ya jotoardhi,” amesema.

Post a Comment

0 Comments