Ticker

6/recent/ticker-posts

VYAMA PINZANI VITOE MCHANGO KWENYE MAANDALIZI YA DIRA YA TAIFA


*********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

VIONGOZI wa vyama vya pinzani vya siasa wametakiwa kutoa ushirikiano wa dhati katika kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la uhamasishaji wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akifungua mkutano wa uhamasishaji wa ushiriki wa wadau katika maandalizi ya dira hiyo, mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema viongozi vyama pinzani wanahitajika kutoa mchango wao ili inapotengenezwa dira hiyo itawaezesha hata wao kutembea nayo pindi watakapoingia madarakani.


"Viongozi wa vyama pinzani tunahitaji mchango wenu ili tunapoitengeneza hii dira, hapo baadaye hata kama ninyi mtashika madaraka mtembee nayo katika uongozi wenu, iwe ni dira ambayo imejumuisha makundi yote" amesema.


"Tanzania ni yetu sote, kila mmoja anapaswq kutoa mchango wake inavyostahiki, wasitokee wengine wakajiona kuwa wana haki zaidi dhidi ya wengine, sisi sote ni wajenzi wa nyumba moja hakuna haja ya kugombania fito " amesisitiza Kindamba.


Aidha amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo inagusa makundi yote hivyo matarajio ni kwamba kutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wadau wote katika ngazi zote zikiwemo taasisi za elimu juu ya utafiti, sekta binafsi, asasi za kiraia pamoja na wananchi mmoja mmoja.


Kindamba amefafanua kwamba mbali na hilo pia kuwepo na ushirikishwaji wa wadau utakaowezesha kupata dira jumuishi kukidhi mahitaji stahiki ya Taifa katika kipindi cha miaka 25 ijayo.


"Katika Mkoa wetu wa Tanga wajumbe watapata nafasi ya kutoa nakala za vitabu vya dira ya mwaka 2025, vipeperushi na mabango kuhusu maandalizi ya ya dira 2050 ikiwa ni pamoja na kutembelea kwenye vyombo vya habari ndni ya Mkoa ili kutoa elimu" amesema.


"Kwa hakika hii itasaidia kuongeza wigo wa uelewa wa jambo hili kwa watu wote watakaofikiwq na habari hiyo, pamoja na kuacha nyenzo zitakazosaidia kuendelea na uelimishaji wa umma baada ya wajumbe hao kuondoka" amebainisha.


Vilevile Kindamba ameeleza kuwa maandalizi ya dira hiyo yameanza mapema ikizingatiwa kuwa dira inayoendelea kutekelezwa kupitia mpango watatu wa maendeleo ya Taifa ya miaka mitano kwa mwaka 2021/22 ,hadi 2025/26 ambayo itafikia ukomo wake mwaka huu.


Hata hivyo baadhi ya wajumbe wameeleza kuwa dira ya miaka 25 iliyopita imefanya mengi makubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo maboresho makubwa ya miundombinu lakini pia kikubwa kwa upande wa elimu ambapo baada ya kuwepo na elimu bure wanafunzi wote wameweza kupata elimu.


"Dira iliyopo ya miaka 25 iliyopita imeweza kuwafanya watoto wote mijini na vijijini kupata elimu bure tofauti na zamani ambapo wazazi walilazimika kulipa ada hivyo kufanya wengi kushindwa kwenda shule" amesema Ramadhani Mohamedi.


Naye Shabani Ngozi amesema, "maendeleo yapo na tunayaona lakini ni maendeleo ya vitu na siyo wananchi, kama viongozi bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili wananchi wa Tanzania wanufaike na dira ya maendeleo ya mwaka 2050".




Post a Comment

0 Comments