Ticker

6/recent/ticker-posts

WEZI 11 WA MITANDAONI WAKAMATWA TANGA, RPC AONGEA

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WATUHUMIWA 11 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Tanga kwa kujihusisha na utapeli na wizi wa mitandaoni huku wakiwa na vifaa mbalimbali vya kufanyia uhalifu huo pamoja na fedha za kigeni.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, SACP Henry Mwaibambe amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Hadija Nyange (35) mkazi wa Wilaya ya Muheza, Zaina Athumani (25) mkazi wa mtaa wa Msambeni jijini Tanga, Omari Mohamedi (27) mkazi wa Mkanyageni, Tanga,

Wengine ni Innocent Omeme (35), Abdulazizi Nzori (31), Said Hassan (24), Rashid Habibu (23), Said Juma (30), Iddi Kaniki (35), David Rupiana (22) na Salum Rajabu (24), wote wakazi wa Dar es salaam.

Aidha Kamanda Mwaibambe alisema, "watuhumiwa walikamatwa maeneo ya Donge jijini Tanga ambako walipangisha chumba kwa mkataba wa mwezi mmoja kulipa kiasi cha sh 800,000" amesema.

"Lakini hao pia walikutwa na pesa taslimu sh 2,085,300, pesa ya Congo sh 45,100, pesa ya Marekani dola 1, simu kubwa 11 aina mbalimbali pamoja na simu ndogo za kitochi 13 aina mbalimbali, kadi 42 za simu, katarasi 43 zilizoandikwa namba za simu na majina ya mawakala lakini pia kadi 5 za benki za Crdb, Nmb, Posta na Chapchap" amefafanua.

Hata hivyo amesema baada ya kufanya uhalifu wao walikuwa wakichoma moto laini za simu ambazo wamekwisha zitumia lakini pia walikutwa na namba za simu mbalimbali 441 ambazo wameziandika kwa ajili ya kutapeliwa.

Kamanda amesisitiza kwamba namba za simu 183 zilitumiwa ujumbe wa kutakiwa kutuma hela na 42 zilikuwa kwenye mchakato ambapo wakishafanya utapeli wanaweka alama ya tiki kwenye namba husika na kwa ambaye yuko kwenye mchakato wanaweka herufi H.

Wakati huohuo, jeshi hilo limewatia mbaroni watuhumiwa wengine watatu waliokuwa wakisafirisha dawa za kulevya mirungi mabunda 313 ambayo yana uzito wa kg 112.5 katika barabara ya Same -Korogwe, eneo la Chekelei kata ya Mombo.

Kamanda amewataja watuhumiwa kuwa ni Samiru Shemweta (39) ambaye ni dereva, Abdallah Mndumi (37) wote wakazi wa Sakina Arusha na Abdulazizi Bakari (34) mkazi wa Chamazi, Dar es salaam.

"Watuhumiwa wamekutwa eneo la Chekelei wakiwa kwenye gari yenye namba T 467 CJS aina ya Toyota Carina wakiwa na bunda 313 za mirungi yenye kilo zipatazo 112.5 na tunawashikilia, taratibu za kuwafikisha mahakamani zinafanyika" amesema.

Katika tukio jingine mtu mmoja alijulikana kuwa ni Elias Ndekelo (27) mkazi wa Lukozi, wilani Lushoto anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kumshambulia na kumuua Paulo Daniel (35) mkazi wa Hambalawei kutokana na wivu wa mapenzi baada ya kuwa walikua wakichangia mwanamke.

Kamanda alisema siku ya tukio marehemu alikwenda kulala kwa mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, lakini mtuhumiwa alimuona ndipo akamfuatilia na kujificha, "wakati marehemu anatoka chooni ndipo mtuhumiwa alipomvamia na kuanza kumshambulia kwa panga na kusababisha kifo chake" amesema.

"Chanzo ni wivu wa mapenzi na kwa mujibu wa mtuhumiwa mwenyewe amedai kuwa alihisi mwanamke ana mapenzi zaidi na marehemu na sio yeye, hivyo akaamua kuchukua maamuzi ya kupelekea kifo chake" amesisitiza Kamanda Mwaibambe.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga SACP Henry Mwaibambe akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kamanda Mwaibambe akionesha simu zilizokuwa zikitumiwa na weI wa mitandaoni kutapeli watu.



Waandishi wa habari Mkoa wa Tanga wakimsikiliza Kamanda Mwaibambe.

Post a Comment

0 Comments