Ticker

6/recent/ticker-posts

KINANA ASHAURI UHURU WA KUSEMA UWE NA MIPAKA


*Akumbusha darasa la Hayati Mwalimu Nyerere kuhusu uhuru bila ya nidhamu


Na MWANDISHI WETU


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amesema ingawa inchi ina uhuru mkubwa wa kusema na kutoa maoni, lakini ni vyema ukazingatia mipaka.

Kinana ameyasema hayo leo Agosti 22, 2-23 jijini Dar es Salaam wakati katika mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).


“Mimi nadhani uhuru wa kusema upo lakini kila uhuru una mipaka yake, Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) alikuwa akitufundisha kwamba uhuru bila ya nidhamu ni wendawazimu na nidhamu bila ya uhuru ni utumwa, kwa hiyo kila uhuru lazima uwe na mipaka yake lakini nadhani kwa ujumla uhuru upo wa kutosha wakati mwingine labda kuna kasoro katika utekelezaji wake nadhani ndio maana Watanzania wanapiga kelele katika kusimamia sheria zinazowapa Watanzania uhuru wa kusema.


KUHUSU KATIBA MPYA,
HAKI KATIKA UCHAGUZI


Akizungumzia hilo amesema jitihada zimekuwa zikifanyika kwa muda mrefu katika awamu mbalimbali, lakini Rais Dk. Smia Suluhu Hassan ameonyesha dhimira na kutekeleza kwa vitendo kuhakikisha linafanikiwa.


“Kuna hili jambo linalozungumzwa mara kadhaa juu ya katiba, umuhimu wa kuwepo katiba mpya, kumekuwepo na jitihada nyingi sana, kumekuwepo na tume nyingi, kumekuwa na Tume ya Nyalali, Tume ya Kisanga, Tume ya Warioba na zote hizi ni juhudi za kutafuta Tanzania kuwa na katiba mwafaka, katiba nzuri itakayowapa Watanzania uhuru wa kuamua kushiriki katika mambo yao kwa uhuru mkubwa zaidi.


“Matokeo ya tume hizi kuna baadhi ya mambo yalitekelezwa na mengine hayakutekelezwa na hivi karibuni kumekuwa na mazungumzo ya kuamua mchakato wa katiba.


“Lazima nikiri kwamba awamu hii tangu imeingia madarakani juhudi zimeanza kufanyika na mtakumbuka hata wakati mheshimiwa Rais anahutubia mkutano wa baraza la vyama vya siasa, mkutano wa kituo cha Demokrasia (TCD) na hata alipokuwa anafungua mikutano ya hadhara, alisema juu ya namna serikali yake ilivyojipanga kuhakikisha tunakuwa na katiba na hata sasa hivi kwa kadri ninavyoelewa kuna mchakato wa aina mbili unafanyika.


“Mchakato wa kwanza ni wa kutafuta namna ya kupata katiba, lakini kwa sababu mchakato huu utachukua muda kuna mchakato wa pili ambao ni wa kurekebisha maeneo matatu ambayo yanahusu uchaguzi, huu ni kwa ajili ya uchaguzi wa 2024 na 2025,” alisema.


Alisema sheria hizo tatu zitatazamwa upya ili zijibu matakwa ya hali halisi ya demokrasia kwa hali ya sasa.


“Ya kwanza ni sheria inayohusu tume ya uchaguzi, yapili ni sheria inayohusu uchaguzi wenyewe utakavyoendeshwa nay a tatu ni sheria inayohusu namna vyama vya siasa vitakavyosimamiwa.


“Mimi nina hakika sheria hizi tatu zikitazamwa na sote kwa pamoja tukikubaliana kupitia vikao kama hivi kupitia TCD na baraza la vyama nina hakika tutakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki zaidi kuliko wakati wowote mwingine kutoa nafasi kwa Watanzania kuwachagua wale ambao wangependa wawe wawakilishi katika vyombo vya uwakilishi,”


“Kwa hiyo je demokrasia imekuwepo, mimi naamini naam imekuwepo kwa kutazama namna idadi ya wawakilishi wa vyama ilivyokuwa ikiongezeka, je kuna kasoro, naam kasoro zipo na ndio mana tunakutana humu ndani na tutakutana katika baraza la vyama kushughulikia kasoro hizo kuzisahihisha, je dhamira kwenye awamu hii ipo, naam nadhani dhamira ipo na ni muhimu kushirikiana tufikie dhamira hiyo, tupate sheria nzuri na hasa sheria zinazosimamia uchaguzi, tume ya uchaguzi na sheria ya vyama ili uchaguzi ujao wa 2024/2024 uwe wa haki zaidi,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndug, Abdulrahman Kinana akizungumza leo Agosti 22, 2-23 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).(Picha na Fahadi Siraji)


Post a Comment

0 Comments