Ticker

6/recent/ticker-posts

MAENEO YENYE MAJI MENGI ARDHINI YATANGAZWE KAMA MAENEO TENGEFU -MHANDISI ARON



Na Okuly Julius-Dodoma 


MKURUGENZI wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph, amesema changamoto iliyopo katika maeneo yenye maji chini ya ardhi ni kutotangazwa kama maeneo tengefu na ndio sababu ukitaka kwenda kuchimba utakuta tayari yana wamiliki.

Amebainisha kuwa maji chini ya ardhi ni fursa muhimu lakini inakuwa ngumu kuyafikia kwa sababu maeneo husika yanamilikiwa, hivyo kuongeza gharama kuyafikia.

Hayo ameyaeleza Leo Agosti 11,2023 jijini Dodoma wakati wakati akiwasilisha taarifa ya utendajikazi wa mamlaka hiyo kwa ujumbe wa Bodi ya Taifa ya Maji, ulioongozwa na mwenyekiti wa bodi hiyo, Mhandisi Mbogo Mfutakamba, walipotembelea ofisi za mamlaka hiyo.

"Katika mabonde tisa ya maji yaliyopo nchini, maji yanayozungumziwa ni yale ambayo yanaonekana juu ya ardhi na sio yaliyopo chini ya ardhi ambayo ni tegemeo kubwa kwa Mkoa wa Dodoma ila changamoto kubwa ni kuwa maeneo mengi hayo yanamilikiwa na Watu hivyo gharama ya kulipia fidia ni kubwa ni vyema maeneo hayo yakawa maeneo tengefu,"ameshauri Mhandisi Aron

Mbali na hayo Mhandisi Aron ameeleza namna usomaji mita shirikishi ulivyosaidia kupunguza kiwango cha upotevu maji.

Amesema usomaji huo umewezesha kubaini uhalisia wa kiwango cha maji alichotumia mtumiaji na kiwango cha ankara ya maji alichotozwa mteja wa mamlaka hiyo.


"Ushirikishwaji wananchi wakati wa usomaji mita umesaidia sana kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kwani tunaweza kufahamu kiwango halisi ambacho mtumiaji alichotumia na ankara aliyotozwa.

Ameongeza kuwa: "Kupitia utaratibu huo, mtumiaji anatumiwa ujumbe mfupi unaoeleza kiwango cha maji alichotumia na kama atakuwa na tatizo anaweza kukata rufaa kabla ya kiwango hicho kuchakatwa."

Amesema mamlaka hiyo pia inatumia mfumo wa upigaji picha mita ya mteja kisha kutumwa kwa mamlaka ili kuhakiki kama mita husika imesomwa kwa usahihi.

Mhandisi Joseph amebainisha kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma.

Mwenyeti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Mhandisi Mbogo Mfutakamba, alisema maendeleo ya uchumi wa dunia yanategemea na upatikanaji maji ya uhakika.

Amesema kwa sababu hiyo uwekezaji mkubwa unahitajika kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa.

"Zamani suala la utunzaji vyanzo vya maji ilikuwa jambo gumu kueleweka lakini sasa suala hilo limeanza kupewa kutiliwa mkazo," alibainIsha.

Mhandisi Mbogo alieleza kuwa serikali imeipa nguvu bodi hiyo kuhakikisha maji yanaendelea kuwepo kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA, Balozi Job Masima, Mjumbe wa bodi hiyo, Peter Mavunde, alisema DUWASA itaendelea kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanaendelea kupata huduma ya maji.

Aliwataka wataalamu wa mamlaka hiyo kuendelea kutumia ujuzi wao kusaidia wananchi waendelee kupata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu na DUWASA katika kutatua changamoto mbalimbali pindi zinapojitokeza.

Naye, Mjumbe wa Bodi ya DUWASA, Profesa Davis Mwamfupe alisema watumiaji wa maji wanapaswa kuwa wa kwanza katika utunzaji vyanzo vya maji.

"Wananchi wafahamu kwamba wao ndio wa kwanza kujiuliza jitihada walizozifanya katika kutunza vyanzo vya maji pindi yanapoadimika na sio kuanza kulaumu mamlaka za maji," alieleza Profesa Mwafupe ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma.

Post a Comment

0 Comments