Ticker

6/recent/ticker-posts

TAASISI ZITAKAZOFANYA UNUNUZI NJE YA MFUMO FAINI NI TSh. MILIONI KUMI


Na mwandishi wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA imesema Taasisi yoyote ya Umma itakayofanya Ununuzi nje ya Mfumo wa NeST itatozwa faini ya kiasi kisichopungua Milioni kumi.

Akizungumza katika Mafunzo wezeshi ya utumiaji wa mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya mtandao (NeST) yanayoendelea kutolewa jijini Dodoma Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA Bw. Eliakim Maswi amesema kuwa suala la kuanzisha Mfumo huu wa kuendesha michakato ya zabuni za umma ni suala mtambuka na kwamba ni wajibu kwa taasisi zote za umma kujifunza mfumo ili kuweza kuutumia kwa usahihi.

“Napenda ieleweke kuwa Serikali inaziwajibisha taasisi zake kutumia mfumo huu wa Ununuzi, hivyo michakato yote ya kufanya ununuzi wa umma serikalini, ni lazima ifanyike kupitia mfumo wa NeST” Alisema Maswi

Sambamba na hilo Bw. Maswi ameongezea kuwa endapo Taasisi yoyote ya umma itafanya Ununuzi nje ya Mfumo itakumbana na adhabu ya kutozwa faini isiyopungua kiasi cha Tsh Milioni 10 kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na taratibu za Ununuzi wa umma.

“lakini pia mtambue kuwa kwakuwa kuna ulazima kwetu sisi taasisi za umma kufanya ununuzi kupitia mfumo huu basi muelewe pia kuwa kuna adhabu itakayotolewa kwa kila taasisi ambayo itathubutu kufanya Ununuzi nje ya Mfumo wa NeST”. Aliongezea.

Mafunzo kwa ajili ya matumizi ya mfumo huo yanaendelea kutolewa kwa maafisa wa taasisi za umma katika mikoa mbalimbali nchini huku ikielezwa kuwa mpaka ifikapo tarehe moja Oktoba ambapo matumizi ya mfumo wa NeST kwa ajili ya kufanya Ununuzi wa Umma yataanza rasmi na hakutakuwa na Shughuli yoyote ya ununuzi wa Umma itakayofanyika nje ya Mfumo wa NeST.

Post a Comment

0 Comments