Ticker

6/recent/ticker-posts

TEMESA NA TRA ZASAINI MKATABA WA UTOAJI HUDUMA ZA MATENGENEZO

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwishoni mwa wiki iliyopita, zimesaini mkataba wa utoaji wa Huduma za Matengenezo (Service Level Agreement) mkataba ambao unahusisha matengenezo ya magari, mitambo, umeme. Elektroniki, matengenezo ya kangavuke pamoja na TEHAMA.

Tukio la utiaji saini mkataba huo limefanyika katika hoteli ya Morena iliyoko Mkoani Morogoro na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Mamlaka ya Mapato Tanzania Moshi Kabengwe.

Mamemeja wa Mikoa wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) na Mameneja wa Mikoa wa Mamlaka ya Mapato Tanzaia (TRA) kote nchini wamesaini mikataba hiyo ya utoaji wa huduma za matengenezo na kuahidi kusimamia makubaliano yaliyoingiwa katika mikataba hiyo kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa pande zote mbili.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda amesema, TEMESA imesaini mkataba huo na TRA kwa lengo la kutoa huduma bora, yenye tija na kwa wakati unaostahili na kueleza kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na kusaini mkataba huo ni kuongeza tija katika makusanyo kwa kuwa malipo yatakuwa yakipatikana kwa wakati na hivyo kurahisisha ulipwaji wa madeni kwa wazabuni wanaosambaza vipuri vya matengenezo hayo.

Mhandisi Karonda pia amewataka mameneja wa Wakala huo kuhakikisha wanatimiza matakwa ya kimkataba kama yanavyohitajika ili kutimiza malengo hayo.

''Wito wangu kwa mameneja wote ni kuhakikisha wanatimiza matakwa ya mkataba kama ulivyoelekeza ili kuweza kuleta tija iliyokusudiwa kwa sababu tunao wazabuni wa kutosha, tunao mafundi wenye uwezo, tunazo karakana nzuri, tunavyo vitendea kazi vya kuweza kufanya kazi kwahiyo tunategemea kuwapa huduma nzuri'' Amesema Mhandisi Karonda.

Aidha, Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Moshi Kabengwe, akizungumza katika tukio hilo amesema lengo la kusaini mkataba huo ni kuboresha huduma ya vyombo vya moto vya Mamlaka hiyo, kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati,uharaka na urahisi ili kuiwezesha Mamlaka hiyo kutenda shughuli zake za ukusanyaji mapato ya Serikali kwa uhakika.

''Tuliona ili kuweze kuwa na ufanisi na malengo ambayo yamekusudiwa kufikiwa, mkataba huu usainiwe kati ya Meneja wa Mkoa wa TEMESA pamoja na Meneja wa Mkoa wa Kikodi wa TRA ili wahakikishe wanaenda kusimamia kwa pamoja mikataba hiyo na kusimamia utekelezaji wa mkataba huo kwa ufanisi.'' Amesema Kabengwe na kuwataka mameneja hao kwa pamoja kuhakisha wanasimamia kikamilifu mikataba hiyo ili malengo ya kusaini mikataba hiyo yaweze kufikiwa kwa wakati, na gharama nafuu.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro James Jilala Kasamalo akizungumza baada ya kusaini mkataba amesema, mkataba huo utawasaidia katika ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuwa mkataba huo umeeleza wajibu wa kila mmoja namna ambavyo atatenda shughuli zake kwa ufanisi.

Aidha Meneja wa TEMESA Simiyu Mhandisi Moses Humbe amesema anaamini litakapokuja suala la utekelezaji, mkataba huo utakuwa na tija kwa pande zote mbili kwakuwa kazi za Mamlaka hiyo kuanzia sasa hazitakwama kwani Wakala huo tayari umejipanga kuhakikisha vipuri vyote vinavyohitajika kwa ajili ya matengenezo ya magari yao ili waweze kukusanya mapato ya Serikali vitapatikana kwa wakati na wataweza kutimiza majukumu yao kwa ukamilifu.


Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Sunday Kyungai kushoto na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro Bwn. James J. Kasamalo kulia wakisaini mkataba wa utoaji huduma za matengenezo ya magari, mitambo, umeme, elektroniki na TEHAMA huku wakishuhudiwa na Mamemeja wa Sheria kutoka TEMESA NA TRA, Ismail Manjoti kushoto wa TEMESA na Primi Telesphory wa TRA. Tukio la utiaji saini lilifanyika mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Morena iliyoko Mkoani Morogoro.

Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi kushoto na Naibu Mkurugenzi wa Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi Tija Ukondwa kulia wakisaini mkataba wa utoaji huduma za matengenezo ya magari, mitambo, umeme, elektroniki na TEHAMA huku wakishuhudiwa na Mamemeja wa Sheria kutoka TEMESA NA TRA, Ismail Manjoti kushoto wa TEMESA na Primi Telesphory wa TRA. Tukio la utiaji saini lilifanyika mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Morena iliyoko Mkoani Morogoro.

Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Liberatus Bikulamchi kushoto na Meneja Usimamizi wa Huduma za Utawala Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yassin M. Mwita kulia wakipeana mikono baaada ya kusaini mkataba wa utoaji huduma za matengenezo ya magari, mitambo, umeme, elektroniki na TEHAMA. Tukio la utiaji saini lilifanyika mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Morena iliyoko Mkoani Morogoro. Picha ya pamoja, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Hassan Karonda (watatu kushoto waliokaa) na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bwn. Moshi Kabengwe (watatu kulia waliokaa) mara baada ya kushuhudia tukio la utiaji saini mkataba wa utoaji huduma za matengenezo ya magari, mitambo, umeme, elektroniki na TEHAMA. Nyuma yao ni baadhi ya watumishi kutoka TRA na TEMESA.

PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO TEMESA

Post a Comment

0 Comments