*Atoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu uamuzi wa Mahakama
*Aelezea ushiriki wa Bunge na muda uliotolewa kujadili
*Aweweka wazi sheria zinazotumika mikataba ya kimataifa
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WAKILI maarufu nchini Alex Mgongolwa amejitosa kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa Mahakama kuhusu sakata la bandari na namna mkataba wenyewe ulivyo.
Katika ufafanuzi wake Wakili Mgongowa amefafanua hatua kwa hatua lakini katika baadhi ya maelezo yake ameweka wazi haiwezekani kutumia sheria za ndani ya nchi kuzungumzia sheria za mkataba wa kimataifa.
Wakili Mgongolwa ametoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na kituo cha redio cha Clouds FM kupitia kipindi chake cha Power breackfast ambapo ametoa ufafanuzi katika hoja zilizotolewa na waliopeleka shauri mahakamani na uamuzi wa Mahakama.
“Kuhusu mkataba wa bandari kilichokuwa kinashindaniwa jumla kulikuwa na mambo sita .Baadhi ya mambo yaliyokuwa yanabishaniwa je ule mkataba wa bandari ni mkataba?
“Lingine ni je mkataba huu hauhatarishi utaifa wa taifa la Tanzania na kulikuwa na maneno ambayo yanatumika kusema kwamba bandari imeuzwa , nini kimeuzwa tumetoa uhuru wetu na kadhalika
“Kingine kilichokuwa kinabishaniwa ni je mkataba huu unatawaliwa na sheria zetu za kawaida, sheria za mkataba za kawaida hapa nchini na kwanini uhalali wa kusema mashauri au migogoro katika mkataba huu iende ikatatuliwe Afrika Kusini na sio hapa.
“Kwa hiyo kimsingi kabisa ukikuta suala la kikatiba hasa lililokubwa ni hilo linalozungumzia kuhusiana na utaifa kwamba mkataba huu unakiuka utaifa kama ulivyotamkwa kwenye Katiba , huu ndio mgogoro uliokuwepo,”amesema wakati anaanza kutoa ufafanuzi.
Wakili Mgongolwa amesema ukienda moja kwa moja kwenye huo mkataba hasa viini vya ushindani katika mgogoro huo ni kwamba mkataba huo kwa kiasi kikubwa unaangilia je hukumu imejikita kwenye ushiriki wa umma katika kupitishwa huo mkataba?
“Mkataba uko bungeni kwasababu kwa vyovyote vile yale majadiliano ya mwanzo umma haukushiriki, haukupaswa kwa mujibu wa kuweza kuzungumzia hiyo mikataba na kufichua mikataba…
“Lakini kipo kipengele kwenye kanuni za Bunge ama ambacho kinaiwezesha Bunge likaamua kushiriki kwenye hili suala. Hasa ukiangalia ile taarifa ilikuwa ni ya siku moja ,saa 24.
“Taarifa ilikuwa inatoa mwito watu kushiriki kutoa mawazo yao, waleta hoja au waliopeleka shauri mahakamani walikuwa wanasema huo ni muda mfupi sana wa saa 24 ukiangalia ukubwa wa mkataba huu wenyewe na ukiangalia umuhimu wa mkataba wenyewe.
“Hata hivyo kanuni haziweki ukomo wala hazizuii ni wakati mwingine sheria inaweza kupita bila kupitia huu mchakato wa kusikiliza umma , hivyo ni ridhaa ambayo ni hiyari ambayo imetolewa kwenye kanuni za Bunge zenyewe.
“Kwa hiyo wale waleta hoja walikuwa wanazipinga zile kanuni kwa maana ya ule muda uliotolewa ulikuwa ni kidogo kwa hiyo neno lililokuwa likitumika muda ulikuwa kidogo lakini Mahakama yenyewe ikasema tazama ule muda…
“Lakini naangalia kiini pia cha hili hitajio la muda linatokana na nini, kwamba hili limetokana na kanuni , nini msimamo wa sheria kuhusu kanuni za Bunge kwa maana ya kuzihoji , ikaangalia ikaona uamuzi ulitokea katika nchi mbalimbali India ikiwa mojawapo.
“Na wanazuoni mbalimbali wale wanasheria waliowahi kuandika wanasema kanuni hazishindaniwi au huwezi ukazipinga katika Mahakama yoyote pamoja na hii Mahakama ya Kati hazipaswi kuhojiwa,”amesema.
Ameongeza dhana au mantiki ni kwamba liache Bunge liendeshe shughuli zake bila kuingiliwa kwa namna yoyote , kama ambavyo Mahakama inavyodai uhuru wa kutoingiliwa katika kufanya maamuzi.
Amesema au kama Serikali ambavyo inataka iendeshe mambo yake bila kuingiliwa akitoa mfano ukitaka kumuingilia polisi akitaka kukumata atakwambia umemzuia kufanya kazi yake.
“Kwa hiyo dhana hiyo ya ulinzi ya utendaji kazi wa vyombo hivi vya Serikali ndio iko hivyo kwa hiyo wakosoaji katika hili wanasema haiwezekani mkaachiwa au mkafanya vitu vyote mnavyotaka bila kujali maslahi ya umma.
“Lakini Mahakama inasema isubiriwe kwanza.Nini msimamo wa sheria kuhusu kanuni hizi?Kanuni hizi zinahojiwa au hazihojiwi , jibu likawa kanuni hizi hazihojiwi na tusingependa kuingiza vidole vyetu kwenye kanuni ambapo msimamo wa sheria unafahamika.
“Afrika Kusini wao wameandika kabisa kwenye Katiba yao hakuna sheria itakayopita bila ushiriki wa umma , ushiriki huo wa umma uwe na muda ambao unajitosheleza.Hata hivyo kujitosheleza kwa muda kunategemea,
“Kwa mfano Katiba yenyewe mkitaka kuijadili ili muweze kubadilisha muda unaohitajika utakuwa muda mrefu zaidi kuliko sheria ya manunuzi ya mali za umma, sheria ambazo ni za kitu fulani.
“Kipendelea cha muda ushiriki wa umma kimewekwa wazi na Mahakama imesema mkataba huu ni halali kwa maana ya namna ambavyo uliweza kujadiliwa na kupitishwa kule bungeni…
“Na kwamba Bunge lilikuwa na Mamlaka ya kufanya vile kwa mujibu wa Katiba yenyewe kwamba mikataba ya aina hii kwa mujibu wa vipengele vya ibara za Katiba inaonyesha mkataba ni lazima upate ridhaa kutoka bungeni
“Kwa hiyo utaratibu ule wa upatikanaji wa ridhaa bungeni , utaratibu ule ndio uliozungumziwa sana, utaratibu ule ulikuwa ni sahihi na haukukiuka kipengele chochote cha Katiba.
“Kifungu kingine kilichoangaliwa sana ni mkataba ule ukiuangalia utakuta hauna thamani ya kipesa au ya kifedha ambayo kisheria huwezi kuchukuliwa ndio msingi unaohalalisha mkataba(Consideration).
“Sasa walikuwa wanasema ukiangalia huu mkataba haina hiyo.Lalamiko kuwa huu mkataba utamkwe kwamba si mkataba kwasababu haujakidhi hilo hitajio ambalo lipo kwenye sheria yetu ya mikataba.
“Ndio walalamikaji wanasema , ili uwe mkataba kipengele kinasema lazima kuwe na thamani ya pesa. Huu ni mkataba ambao huzioni namba , huzioni fedha kwa hiyo walalamikaji walikuwa wanasema utamkwe huu si mkataba halali, haukidhi mahitajio ya kifungu cha 25 cha sheria zetu za mikataba.
Wakili Mgongolwa amesema Mahakama imeeleza jambo la msingi kwamba mkataba huo wa kimataifa ni tofauti na mikataba ya ndani ya nchi , yaani mikataba ya kimataifa haitafsiriwi kwa sheria za ndani ya nchi.
“Kwasababu mikataba ya kimataifa yapo makubaliano ya kimataifa ambao yenyewe ndio inaotafsiri mikataba yote ya kimataifa, kwa hiyo ni makosa kutafsiri mkataba wa kimataifa kwa kutumia sheria za ndani.
“Eneo hili la mikataba ya kimataifa ni jipya ,sio eneo la muda mrefu, sayansi ya sheria ya mikataba ya kimataifa ni mpya na ndio maana utaona watu wengi wanasheria wanagombana kuhusiana na tafsiri hizi…
“Kwasababu wengine wanataka kutumia mikataba hii ya kimataifa kutafsiri kwa kutumia sheria za ndani. Hapa mikataba ya kimataifa ina ulimwengu wake ambao unatumika katika kuitafsiri , ukiangalia ule mkataba wa kimataifa yenyewe inaeleza tafsiri yake inaungwa mkono na nini
“Hoja nyingine ilikuwa walalamikia kuhusiana na matumizi ya sheria ya manunuzi ya umma sasa ukitumia sheria ya manunuzi ya umma kwenye mkataba wa nchi hiyo hapana,”amesema Wakili Mgongolwa ambaye ametoa ufafanuzi wa kirefu kuhusu uamuzi wa Mahakama katika kuzungumzia mkataba wa bandari.
0 Comments