Ticker

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAAHIDI KUENDELEZA MAGEUZI SEKTA YA ELIMU UKEREWE


#Yaipongeza Wilaya kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya Elimu.

#Yakabidhi Meza 50 na Viti 50 Shule ya Sekondari Chief Lukumbuzya.

***
Kaimu Meneja  Benki  ya CRDB Kanda ya Ziwa Ndg. Emmanuel Ndeonasia ameuhakikishia uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza kuendeleza mageuzi ya kimkakati katika uboreshaji wa miundombinu ya Elimu inayoendelea kutekelezwa na kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuboresha zoezi la ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.

Ameyasema hayo Septemba 6, 2023 wakati akikabidhi Meza za kusomea wanafunzi hamsini (50) na Viti hamsini (50) katika Shule ya Sekondari Chief Lukumbuzya iliyopo Kitongoji cha Kamote, Kijiji cha Muriti, Kata ya Muriti Wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza.


"CRDB tumekuwa tukifanya hivi katika Wilaya tofauti tofauti kwa upande wa Elimu na Afya, tupo hapa kuhakikisha kwamba tunakabidhi Meza 50 na Viti 50 kama faida ambayo sisi Benki ya CRDB tumeitengeneza" ,amesema Ndeonasia.

Amesisitiza kuwa, kutokana na ushirikiano uliopo kati ya halmashauri na Benki ya CRDB wataendelea kutoa mchango wao katika maeneo mbalimbali yenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwapunguzia mzigo wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya Elimu na Afya.

Katika hatua nyingine, Ndeonasia amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Emmanuel L. Sherembi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe. Joshua B. Manumbu kwa kujenga mahusiano imara na Benki ya CRDB hadi kupatikana kwa vifaa hivi, amewahimiza wanafunzi shuleni hapo kuvitunza Viti na Meza hizo ili ziwasaidie na wanafunzi wengine.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Emmanuel L. Sherembi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kurudisha faida katika jamii ili kutatua changamoto zinazoikabili na ameiahidi Benki hiyo ataendelea kushirikiana nayo kwa kuwa anatambua na kuthamini mchango wao katika kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na serikali.

"Nimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotatua kero mbalimbali zinazoikabili jamii hii, tupo tayari kutekeleza miradi yote inayoelekezwa na serikali yetu ya awamu ya sita ili kuboresha Elimu na maeneo mengine, kiupekee niwashukuru Benki ya CRDB kwa kurudisha faida yenu kwa wananchi kama mnavyotukumbuka miaka yote kwa kuleta michango yenu katika Idara mbalimbali zikiwemo Afya na Elimu", amesema Sherembi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Wilaya hiyo Mwl. Evalista Msule ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali, ameiomba Benki hiyo iendelee kutoa msaada huu katika shule nyingine zilizopo katika halmashauri hiyo ili kumaliza changamoto za upungufu wa viti na meza katika shule za sekondari kutokana na wingi wa wanafunzi uliopo katika shule hizo.

Pia, Mwalimu wa taaluma shuleni hapo Mwl. Faraja Mbilinyi ameeleza kuwa shule hiyo ilianzishwa Mwaka Jana 2022 ikiwa na wanafunzi 252 wa kidato cha kwanza na Mwaka huu 2023 shule hiyo imepokea wanafunzi 333 wa kidato cha kwanza na hivyo shule nzima kuwa na jumla ya wanafunzi 584.

Awali, Shule ya Sekondari Lukumbuzya ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa Viti 149 na Meza 133, kutokana na juhudi za Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Ndg. Emmanuel L. Sherembi na uongozi wa Wilaya kwa niaba ya shule hiyo, Mwl. Mbilinyi ameushukuru uongozi wa wilaya hiyo kwa kujenga mahusiano mema na Benki ya CRDB na kufanikisha upatikanaji wa vifaa viti na meza, ameendelea kuuomba uongozi huo uwakumbuke kukamilisha idadi iliyopungua baada ya msaada huu kupatikana ili kumaliza kero ya upungufu wa viti na meza shuleni hapo.

Naye, Diwani wa kata ya Muriti Mhe. Athanas Kiza Marobo ameeleza kufurahishwa na msaada huo, amesema juhudi za Mkurugenzi alizozifanya kupatikana kwa vifaa hivyo ni sawa na Benki hiyo kuwavalisha nguo wakazi wa kata ya Muriti.

"Watoto wetu wamepata furaha kubwa, CRDB mmetuvalisha nguo sisi wakazi wa Muriti, kulikuwa na changamoto kubwa ya viti na meza lakini kwa niaba ya wakazi wa kata hii naipongeza Benki ya CRDB",amesema


Post a Comment

0 Comments