Tanzania imeahidi kuwa itaendelea kuheshimu na kusimamia misingi ya mtangamano wa bara la Afrika kama ilivyofundishwa na kuachwa na waasisi wa Taifa hili, ili kufikia Afrika yenye ustawi na umoja.
Hayo yameelezwa leo Septemba 15, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati anafungua Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar.
Dkt. Biteko aliwambia wajumbe wa kikao hicho ambacho kinalenga kutoa mapendekezo ya kisera na miongozo ya kimkakati katika uendelezaji wa sekta ya miundombinu barani Afrika kuwa, Tanzania ipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ambayo msingi wake ni kuimarisha mtangamano baina ya Tanzania na nchi inazopakana nazo, Afrika na dunia kwa ujumla.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa yenye urefu wa kilomita 1,800 inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilomita 1,400 linalounganisha Tanzania na Uganda, Mradi wa Bwawa la Kuzalisha umeme wa Maji la Julius Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 kwa ajili ya matumizi ya Tanzania na nchi jirani na kufufua shirika la ndege ambalo kwa sasa lina ndege 12 zinazoiunganisha Tanzania na nchi zisizopungua 9 za Afrika.
Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana ili kufikia matarajio ya mamilioni ya Waafrika ya kuwa na miundombinu ya uhakika. Kufanikisha hilo, Dkt. Biteko alitoa wito kwa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, washirika wake na wabia wa maendeleo kuimarisha juhudi za utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ambayo ni muhimu katika kuimarisha biashara, kuongeza ajira na kukuza uchumi barani Afrika.
Awali, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya miaka 10 ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Miundombinu Barani Afrika (PIDA), wajumbe waliainisha masuala mbalimbali ya kuzingatia ili awamu ya pili ya mpango huo, uweze kufanikiwa. Masuala hayo ni pamoja na kuwa na sera zinazoendana na mabadiliko ya dunia, kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu na kupeana taarifa muhimu ili kufanikisha uandaaji na utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya miundombinu.
Kufanyika kwa mkutano huo nchini ni jitihada za Serikali ya awamu ya sita kupitia Ubalozi wake nchini Ethiopia, chini ya uongozi wa Balozi Innocent Shiyo za kukuza diplomasia ya uchumi na utalii wa mikutano.
Wajumbe takribani 400 kutoka barani Afrika; washirika wa maendeleo, kama Benki ya Maendeleo ya Afrika, Exim Bank; Kamisheni ya Uchumi ya Afrika; watafiti na wanazuoni wa fani mbalimbali duniani wameshiriki mkutano huo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisoma hotuba ya ufunguzi wa Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na wajumbe wengine katika meza kuu wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar
Wajumbe wakiimba Wimbo wa Taifa ambao ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo (wa tatu kushoto na Balozi wa Tanzania, Jamhuri ya Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji (wa pili kushoto)
Kamishina wa Miundombinu na Nishati wa Umoja wa Afrika, Bibi Amani Abou-Zeid akihutubia Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar
Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Erick Ngilangwa na Bi. Maria Ndumbalo wakifuatilia kwa makini hotuba za ufunguzi
Wajumbe wakisikiliza hotuba za ufunguzi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiagana na baadhi ya wajumbe wanaoshiriki Kikao cha Umoja wa Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda na ya Bara, na Nishati baada ya kufungua kikao hicho.
0 Comments