Ticker

6/recent/ticker-posts

WASIOJIWEZA WAISHUKURU SHUWASA KUWAPATIA HUDUMA YA MAJI BURE


Na Mwandishi wetu _ Shinyanga

Watu wasiojiweza wakiwemo vikongwe,  wameishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga(SHUWASA), kwa kuwapatia huduma ya maji bure kila mwezi bila kulipia ikiwa ni sehemu ya  uwajibikaji kwa kutoa msaada hali inayorudisha fadhila kwa jamii.


Programu hiyo ambayo ina miaka 10 sasa inanufaisha zaidi ya kaya 35 za Manispaa ya Shinyanga nyingi zikiwa ni za wazee wasio na kipato. 


Wakizungumza wakati wa zoezi la kuwatembelea kwa lengo la kuwafanyia tathimini, wanufaika hao wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwapatia huduma muhimu ya maji bila malipo. 


Elizabeth Bugehu (75) Mkazi wa Bulugalila Manispaa ya Shinyanga,  amesema huduma ya maji bure inamsaidia yeye na mama yake mzazi ambaye anaishi naye kwani hawana uwezo wa kulipia.


"Nilipoambiwa nitakuwa napata maji bure kwa maisha yangu yote niliishukuru SHUWASA na Serikali ya Mama Samia, kwa kunijali na kunipa maji bure. Mimi ni kikongwe na bado ninaishi na mama yangu mzazi ambaye ana miaka zaidi ya 120 na akitaka kuoga nachota maji ya SHUWASA namwogesha, kwakweli tunashukuru sana," amesema Bi. Bugehu. 


Naye Bi. Theresia Stephen (107) mkazi wa Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, ameishukuru Serikali kwa kumuunganishia maji bure na kumruhusu kutumia unit tano bure kila mwezi kwani yeye ni mzee na hana uwezo wa kulipia maji. 


Kwa upande wake Afisa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma kutoka SHUWASA,  Bi.  Nsianeli Gerald, amesema wanufaika hao hupatiwa uniti tano za maji bure ambayo ni sawa na ndoo 250 za lita 20 kila mwezi. 

Amesema hadi sasa wapo wanufaika 35 na watatu kati ya hao waliunganishiwa maji bure na wanaendelea kutumia bila kulipia.


"Zoezi hili ni endelevu na lina takribani  miaka 10 sasa tangu tuanzishe na tathimini  inafanyika kila baada ya miaka mitatu kujua kama wapo waliofariki ili tuweze kuongeza wengine, " amesema Bi Gerald. 

Zoezi la kuwabaini wateja hawa linafanyika kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali za Mitaa na Maofisa wa Ustawi wa Jamii kwa kuweka vigezo muhimu vya kuwatambua ili kuwasaidia kupata huduma ya maji bure.

Post a Comment

0 Comments