Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU: NENDENI MKAWASIKILIZE WANANCHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa maagizo 10 kwa viongozi wa mkoa wa Kagera huku akiwasisitiza wazingatie maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao.

“Viongozi na watendaji wote ninawakumbusha tena wajibu wenu wa kuwatumikia zaidi wananchi, nendeni mkatatue kero zao, wekeni utaratibu wa kuwafuata, kuwasikiliza na kupata ufumbuzi wa kero zao. Wekeni mikakati ya kutatua kero za masuala ya migogoro ya ardhi na makundi mbalimbali katika jamii kama wakulima na wafugaji,” amesema.

Ametoa maagizo hayo leo jioni (Ijumaa, Septemba 22, 2023) wakati akifunga Mafunzo ya siku tano ya Uongozi kwa Viongozi wa Mkoa wa Kagera yaliyofanyika kwenye ukumbi wa ELCT, mjini Bukoba. Mafunzo hayo yaliendeshwa na Taasisi ya Uongozi.

“Kumbukeni kwamba ninyi mnawajibika moja kwa moja kwa wananchi, wasikilizeni na kutatua kero kwa wakati ili waendelee kuiamini Serikali iliyopo madarakani. Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwatumikia wananchi, nasi tuliopewa dhamana ya kumsaidia, kila mmoja atimize wajibu wake ili wote tuwe tunaongea lugha moja ambayo ni kuwatumikia wananchi kwa kuwatatulia kero zao,” amesisitiza.

Maagizo mengine ni pamoja na kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ili kubaini mafanikio ya mafunzo hayo; Mkuu wa Mkoa kuweka mikataba ya utendaji kazi na wakuu wote wa idara na vitengo katika halmashauri zote; watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.

Mengine ni viongozi na watendaji kujiepusha na urasimu usio na tija wakati wa kuwahudumia wananchi; kuhakikisha kunakuwa na usimamizi wa fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na za mapato ya ndani ili zitumike ipasavyo katika maeneo yao; viongozi wote wafuatilie kwa karibu wakandarasi wanaopewa kazi, na iwapo watabaini mapungufu wachukue hatua za haraka badala ya kusubiria viongozi wakuu wapite na kuibua kasoro.

Pia amewataka viongozi hao wazingatie utumishi bora wa umma unaoongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali; watumishi wote katika ofisi zao wafanye kazi kwa kushirikiana, kupendana, kuaminiana na kuepuka fitna na majungu mahali pa kazi na akawataka viongozi waliopewa dhamana wahakikishe wanasimamia watumishi wenzao kupata stahili zao kikamilifu na kuwa wabunifu kwa kutoa motisha ikiwemo za mafunzo kazini.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango wakati akifungua Kongamano la Vijana la Mkoa wa Dodoma ambapo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote waandae makongamano ya vijana ili wabaini fursa zilizopo kwenye mikoa yao.

“Nami nasisitiza Mkuu wa Mkoa na timu yako andaeni mpango mahsusi wa kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Na pia Wakuu wa Mikoa mingine waandae mafunzo kama haya ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bi. Fatma Mwassa alisema lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kujipanga upya kimkakati na kusonga mbele huku wakiongozwa na dhamira ya kutoka hapo walipo.

Alisema changamoto kubwa iliyowasukuma ni hali mbaya ya kiuchumi ya mkoa huo ambao kwa sasa unashika nafasi ya 25 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara huku pato la mwananchi kwa mwaka likiwa ni sh. milioni 1.4 ilhali wastani wa pato la Taifa kwa mwaka ni sh. milioni 2.8.

Alisema kupitia mafunzo hayo, viongozi walioshiriki wamedhamiria kubadilisha utendaji kazi na wameandaa mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ili kuboresha uchumi wa mkoa wao.

Naye Mkufunzi kutoka Taasisi ya Uongozi, Bw. Emmanuel Alfred alizitaja baadhi ya mada zilizowasilishwa kuwa ni Uongozi wa Kimkakati, Maadili ya Viongozi, Afya ya Akili na Uongozi, Itifaki, Majukumu na Uhusiano wa Viongozi Kazini na Usalama wa Nchi na Udhibiti wa Maeneo ya Mipaka kwa kuwa Kagera inapakana na nchi nyingine.

Mada nyingine ni Mahusiano ya Chama na Serikali, Ununuzi ya Umma, Usimamizi wa Matokeo ya Ukaguzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Usimamizi wa Viashiria vya hatari na Udhibiti wa Ndani.

Viongozi walioshiriki mafunzo hayo ni Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Mstahiki Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakuu wa Idara.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua miundombinu katika kituo cha afya cha Kakunyu kilichopo Missenyi, Mkoani Kagera, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa. Kituo hicho kimegharimu shilingi milioni 500, Septemba 23, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi wakati alipokagua miundombinu katika kituo cha afya cha Kakunyu. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi, Septemba 23, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia shehena ya mizigo inayoshushwa kwenye Lori kwa ajili ya kukaguliwa kabla haijavushwa kwenda nchi jirani, wakati alipotembelea Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula ili kuona utendaji kazi wake, Septemba 23, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua shughuli mbalimbali katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye Kituo cha Huduma za Pamoja cha Mutukula, wakati alipotembelea kituo hicho, Septemba 23, 2023. Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments