Ticker

6/recent/ticker-posts

PURA Yaipa Kongole Equinor kwa Kufadhili Upasuaji Wagonjwa wa Ngiri

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeipongeza Kampuni ya Nishati ya Kimataifa ya Equinor Tanzania AS kwa kufadhili utekelezaji wa mradi wa upasuaji kwa wagonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto.

Pongezi hizo zimetolewa leo, Oktoba 06, 2023 Mkoani Lindi mara baada ya PURA kutembelea kambi hiyo maalum ya upasuaji wa ngiri maji na ngiri kokoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi - Sokoine.

Akitoa maelezo kwa maafisa wa PURA waliofika kambini hapo, Afisa kutoka Equinor Tanzania, Dkt. Naomi Makota amesema kuwa kambi ya upasuaji kwa mwaka huu ilianza Oktoba 02, 2023 na itahitimishwa Oktoba 13, 2023. Kambi hiyo kwa mwaka huu, imelenga kuhudumia wangonjwa 200 kutoka Halmashauri ya Manispaa Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.

Dkt. Naomi ameeleza kuwa huu ni mwaka wa tisa tangu Kampuni ya Equinor (iliyokuwa ikijulikana kama Statoil) ianze kufadhili Programu ya NTD ili kuwafanikisha upasuaji wa wagonjwa hao. Mradi huu kwa Equinor ulianza mwaka 2015 Mkoani Mtwara na baadae Lindi mwaka 2017 mpaka leo hii.

Kwa mujibu wa Dkt. Naomi, tangu kuanza kwa utekelezaji wa programu hii, zaidi ya wagonjwa 1600 wa ngiri maji na ngiri kokoto wamefanyiwa upasuaji. Mradi huu hadi sasa umegharimu takribani Dola za Marekani 424,400.


Akizungumza mara baada ya kujionea utekelezaji, Afisa kutoka PURA, Bw. Ebeneza Mollel ameipongeza Kampuni ya Equinor Tanzania kwa kurudisha tabasamu kwa wagonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto, kupitia mradi huu muhimu.


"Kwa niaba ya PURA nitumie fursa hii kuipongeza kwa dhati Kampuni ya Equinor Tanzania kwa kufadhili upasuaji huu. Kwa hakika mradi huu unabadilisha maisha ya wagonjwa na tumeguswa sana na mchango wa Equinor katika eneo hili" aliongeza Bw. Mollel.

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kupitia Kifungu Namba 11 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 kwa lengo la kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Post a Comment

0 Comments