Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA AIPONGEZA NIT KUJIKITA ZAIDI KUTOA MAFUNZO YA AMALI

Na Mwandishi wetu Dar es salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amekipongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kujikita zaidi katika kutoa mafunzo ya amali na kuwaasa kuendelea kuimarisha mafunzo ya hayo katika sekta ya Usafirishaji kwa kuwa ni sekta muhimu sana.

Waziri Prof Mkenda ametoa pongezi hizo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kike wanaosoma programu za uhandisi katika sekta ya usafirishaji pamoja na kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa majengo matano ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa kujenga ujuzi na ushirikiano wa kikanda wa Afrika Mashariki EASTRIP.

Aidha amesema hatua ya kuanza kutolewa kwa mafunzo ya amali kwenye shule za sekondari nchini kutasaidia sana kuwa na Wahitimu wengi wenye ujuzi katika fani mbalimbali ambao watakuwa na uwezo wa kuhudumia miradi ya kimkakati

Amesema lengo la kufanya mageuzi kwenye sera na mitaala ya Elimu nikutaka kuona vijana Wakitanzania wanapata Elimu Bora, shindani inayohitajika kwenye soko la sasa la ajira ndani na nje ya nchi

"Tunataka kuona elimu yetu inazalisha vijana wanaoweza kufanya kazi na si hapa tu Tanzania kama wanavyokuja wataalam kutoka mataifa ya nje basi nasi tunataka tunapokwenda katika nchi za wenzetu tukute vijana wetu wanafanya kazi huko" amesisitiza Prof. Mkenda

Akizungumzia mafunzo ya urubani ambayo yana gharama kubwa nchi za nje amesema yanapotolewa chuoni hapo itapunguza gharama hivyo kuwezesha wanafunzi wengi kupata mafunzo hayo.

Pamoja na hayo, Waziri Mkenda amekitaka chuo hicho kuendelea kusomesha wakufunzi wake katika vyuo vya nje ili kuwafanya wawe bora na wawe na ujuzi, maarifa na uzoefu kutoka katika nchi mbalimbali zilizoendelea na bobezi katika sekta ya usafirishaji ili kuwawezesha kutoa mafunzo ya kitaalam kwa vijana wa kitanzania waweze kuwa shindani kimataifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof Zacharia Mganilwa amesema chuo hicho pamoja na kutekeleza mradi wa EASTRIP lakini pia kimejikita katika kuhakikisha kinasomesha Wakufunzi wake watakaokuwa na uwezo wa kufundisha masomo ya amali katika Chuo hicho.

Baadhi ya wanafunzi wa kike waliopata ufadhili wa masomo katika program za uhandisi kweye sekta ya usafirishaji wameishukiru serikali Kwa hatua hiyo na kwamba Sasa wanakwenda kutumia vizuri fursa hiyo kutimiza ndoto zao ili waweze kutumia taifa.

Mradi wa EASTRIP unaosimamiwa na Wizara ya Elimu, sayansi na teknolojia ni wa kikanda ambao unashirikisha nchi tatu ambazo ni Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya na Ethiopia .

Post a Comment

0 Comments