Ticker

6/recent/ticker-posts

EPIC TANZANIA TOUR YAMPONGEZA RAIS SAMIA, YAFURAHISHWA NA VIVUTIO VYA UTALII VYA SERENGETI


Na John Mapepele

Timu ya Wawekezaji 180 iliyowasili Novemba 4, 2023 kutoka Marekani kwa ziara maalum kupitia programu maalumu ilioanzishwa na kampuni ya utalii ya Gosheni Safari kwa kushirikiana na Serikali ijulikanayo kama ‘Epic Tanzania Tour’ na kupokewa na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi imepongeza jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania za uhifadhi wa raslimali na kutangaza utalii duniani.

Timu hiyo imetoa pongezi hizo baada ya kutembelea Hifadhi ya Serengeti na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku baadhi wawekezaji wakiahidi kurejea kwa ajili ya kutembelea maeneo mengine ya Tanzania na kufanya uwekezaji katika sekta tofauti ikiwemo sekta ya utalii.

Akizungumza leo katika Hifadhi ya Serengeti Kiongozi wa Kampuni iliyoandaa safari hiyo ya Goshen Safari, bwana Peter Robert amesema wawekezaji hao ambao baadhi yao ni mabilionea wenye makampuni makubwa katika sekta za utalii, afya, teknolojia na viwanda wamefurahishwa na vivutio walivyojionea kwenye Hifadhi ya Serengeti na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Rais Samia ya kuhifadhi raslimali za nchi.

“ Naomba kutoa shukrani za dhati kwa kwa Rais kwa kuifungua nchi yetu kipitia filamu ya The Royal Tour ambayo imetusaidia kutuletea wageni hawa kwa kuwa wengi wa wageni kwenye program yetu ya EPIC ni matokeo ya kazi ya mama” . Amefafanua Robert.

Aidha amesifu kazi kubwa inayofanywa na Wizara Maliasili na Utalii ya chini ya Waziri Angellah Kairuki ya kuwashirikisha sekta binafsi katika kutangaza na kuuza utalii wa Tanzania duniani huku akisisitiza kuendelea na ushirikiano huo ili kupata wageni wengi zaidi katika siku zijazo na hatimaye sekta kuchangia zaidi kwenye uchumi wan chi.

Awali akiwapokea wawekezaji hao kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Novemba mwaka huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi aliwataka Watendaji Wakuu wote wa taasisi zinazosimamia uhifadhi na utalii nchini kutoka ofisini na kushirikiana na sekta binafsi katika kuuza na kutangaza utalii kwa manufaa mapana ya nchi yetu.

“Kama Rais wa nchi aliweza kutoka ofisini na kwenda kucheza filamu ya the Royal Tour mimi na wewe ni nani hata tusitoke kushirikiana na sekta binafsi kutembea kwenye maono ya kiongozi wetu mkuu katika kuuza na kutangaza utalii duniani” alihoji Dkt. Abbasi

Aidha, alibanisha kuwa katika mwendelezo wa EPIC Tanzania Tour, mwanzoni wa mwezi Disemba 2023 magwiji wa mchezo wa tennis duniani wataoneshana umwamba katika mchezo huo unaotarajiwa kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Post a Comment

0 Comments