Ticker

6/recent/ticker-posts

PSSSF YATENGA MUDA MAALUM WA MAJUMA MANNE KUSIKILIZA NA KUZIPATIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZA WANACHAMA NCHI NZIMA TANZANIA NA ZANZIBAR.

NA K-VIS BLOG/KHALFANS AID, ARUSHA

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetenga muda maalum wa majuma manne kuanzia Novemba 27 hadi Disemba 22, 2023, kwa lengo la kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za wanachama, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, CPA. Hosea Kashimba, amesema.

CPA. Kashimba amesema hayo kwenye banda la PSSSF katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Novemba 24, 2023.

“Iwapo kuna mwanachama yeyote mwenye changamoto yoyote inayohusu uanachama, michango na mafao, afike katika ofisi za PSSSF zilizo jirani naye Tanzania bara na Zanzibar, tutamsikiliza na kutatua changamoto yake.” Alisisitiza.

Alisema zoezi hilo litakuwa likifanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, Jumatatu hadi Ijumaa.

“Lakini hata baada ya kipindi hicho maalum kufikia ukomo, bado tutaendelea kuwapatia huduma wanachama wetu, lengo hasa ni kuhakikisha wanachama wetu wanafurahia huduma zetu wakati wote.” Alisema CPA. Kashimba.

Pia amerejelea angalizo kwa wanachama na wastaafu, kuwa wasikubali kupokea maelekezo yoyote kutoka kwa watu wasiowajua endapo wanahisi wanachangamoto yoyote kuhusiana na uanachama wao au mafao yao.

“Tunawaasa wanachama wetu hususan wale wanaokaribia kustaafu, watambue kuwa huduma zetu zinatolewa bure bila malipo yoyote, na kama wanachangamoto yoyote wapige simu namba ya bure 0800 110 040 au kupitia mitandao yetu ya kijamii kupitia anuani ya PSSSFTZ.” Alifafanua CPA. Kashimba.
CPA. Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu PSSSF,

Post a Comment

0 Comments