Ticker

6/recent/ticker-posts

WATU 8 WAFA MAJI KATIKA KIPINDU CHA MVUA KUBWA MKOANI TANGA.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

KUFUATIA mvua kubwa za elnino zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Tanga, hadi kufikia sasa watu nane wamepoteza maisha kwa kufa maji.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga (ACP) Almuchius Mchunguzi, ametoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa habari ofisi kwake kwamba watu hao wamekufa maji katika matukio tofauti katika wilaya za Tanga, Muheza, Handeni na Kilindi.


Amewataja watu hao kuwa ni Fabius Masalu (23) mkazi wa kijiji cha Ngomeni na Mbwana Hamisi Makame (48) ambaye ni mgonjwa wa akili alikufa maji katika kijiji cha Kicheba, vyote vya wilayani Muheza.


Wengine waliofariki ni mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Maweni Jijini Tanga aliyefahanika kwa Abubakar Said (7) na Simon Arod mtoto mdogo mwenye umri wa miaka mitatu pamoja na mtoto mdogo mwenye umri wa miaka minane aliyefahamika kwa jina la Nganahe Masefu mkazi wa kijiji cha Mbwagwi wilayani Handeni.


Kamanda Mchunguzi amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuchukua taahadhari na mvua zinazoendelea kunyesha ili wasiweze kupata madhara ikiwemo vifo.


"Mvua zinazonyesha zimesababisha vifo vya watu nane katika mkoa wetu, watu wachukue taahadhari za kiusalama kipindi hiki cha mvua ikiwezekana wahame maeneo ya mabondeni," alisema Kamanda huyo wa Polisi.


Aidha amesema katika hatua nyingine jeshi hilo limefanikiwa kukamata watuhumiwa 107 katika msako waliofanya kwa kipindi cha mwezi mmoja na kwamba watu hao wamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kupatikana na bangi kilo 43, mirungi kilo 123.5 na heroin gramu 242.


Kamanda amebainisha kwamba November 18 mwaka huu walimkamata Hamisi Kombo mkazi wa Kwediboma wilayani Kilindi na wenzake wanne wakidaiwa kujifanya waganga wa kienyeji ambapo walikuwa wakifanya ramli chonganishi katika mtaa wa Pongwe Jijini Tanga.


Hata hivyo Kamanda Mchunguzi amefafanua kwamba watuhumia 41 kesi zao zimepelekwa mahakamani na nyiengine 11 jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi kabla ya watuhumiwa kufikisha mahakamani.


Aidha Kamanda amesema jeshi hilo linawashukuru sana raia wema kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa ambazo zimefanikisha kukamatwa kwa baadhi ya wahalifu pamoja na mali zilizoibiwa.


"Sambamba na hilo, jeshi la polisi linatoa wito kwa waendesha pikipiki (bodaboda) kuchukua tahadhari za kiusalama wanapokuwa kwenye majukumu yao kwa kuhakikisha wanakuwa na mawasiliano ya karibu na madereva wenzao wanapobeba abiria wanaowatilia mashaka,


"Kutokana na wimbi la uhalifu hasa nyakati za usiku, pia kutoruhusu kupokea maelekezo ya abiria, kupakiza mtu mwengine njiani ikiwa ni pamoja na kuchagua njia ambazo siyo salama kwao, lakini pia madereva wote wa vyombo vya usafiri kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali zinazoleta madhara kwa mali na maisha ya binadamu".

Post a Comment

0 Comments