Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO AFUNGA WIKI YA MAONESHO YA UFUGAJI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA DODOMA

Serikali imeitaka Wizara, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwezesha upimaji wa maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akifunga Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko jijini Dodoma.

Amesema wizara hiyo ishirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutenga maeneo ambayo yatatumiwa na wafugaji katika kulisha mifugo yao kwa utaratibu hivyo kuepuka na uharibifu wa mazingira.

Pia, Waziri Jafo ameitaka Wizara ya Maji kupitia Mamlaka za Mabonde nchini kuhakikisha yanalindwa sanjari na kusimamia zoezi la upandaji wa miti katika vyanzo vya maji ili yawasaidie wakulima na wafugaji.

“Vyuo vikuu vya kilimo na mifugo viendeleze tafiti mbalimbali za kuangalia aina ya malisho ambayo yatawasaidia wafugaji wetu kupata malisho ya uhakika kwa ajili ya mifugo,” amesema Dkt. Jafo.

Aidha, Waziri amekipongeza Chama cha Mazingira na Ufugaji Tija Tanzania (CHAMAUTA) kwa kusajili wafugaji nchini na kuwataka kuendelea na zoezi hilo ambalo litasaidia katika kuweka mfumo mzuri wa utunzaji wa mazingira.

Dkt. Jafo ambaye pia ni mlezi wa chama hicho amewapongeza kwa kuweka kipaumbele agenda ya mazingira na kusema Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Amewaomba wafugaji waendelee kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua katika uhifadhi wa mazingira hususan kupitia miradi mikubwa anayotekeleza ikiwemo inayowagusa wafugaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifunga Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Wadau wa mifugo wakiwa katika hafla ya kufunga Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira uliyofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikabidhiwa mche wa mti na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt.. Semistatus Mashimba wakati wa hafla ya kufunga Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments