Ticker

6/recent/ticker-posts

KANALI LABAN: MABADILIKO SERA YA ELIMU, MAJIBU YA CHANGAMOTO ZA UCHUMI

Maboresho ya sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 yana lengo la kuifanya elimu itakayotolewa nchini kukidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya kiuchumi nchini.

Haya yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mh. Kanali Laban Thomas, alipohudhuria Kongamano la thelathini na tatu la Wanazuoni wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania lilifanyika Disemba 13, 2023 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Maboresho haya yanalenga kujibu maswala yote yahusuyo ajira, yamekuja na suluhisho la namna changamoto za utungaji mitaala na namna sahihi ya uandaaji wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu ili waweze kutambua nafasi zao na namna ambayo watashiriki katika uzalishaji mali.” Amesema Kanali Laban.

Kwa upande wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema lugha sio kikwazo kwa mitaala mipya kwani kinachotakiwa ni ujuzi na uzoefu wa waalimu ambao watatumia kuutoa kwa wanafunzi.

“Lugha ya kufundishia si tatizo kwa watoto badala yake ni walimu wanaofundisha kwa kutumia Kiswahili badala ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya sekondari. Kimsingi, walimu hao wanatakiwa wawe na uwezo wa kutoa ujuzi kwa lugha husika na wanafunzi wataelewa na kupata ujuzi pale mwalimu anapokuwa mahiri katika lugha ya kufundishia," amesema Prof. Bisanda.

Aidha, Prof. Makenya Maboko, mhadiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye alikuwa mzungumzaji mkuu amesema wakati umefika ambao Tanzania inahitaji kubadilisha mitaala yake kupitia sera. Pia kuitekeleza mitaala hiyo kupitia elimu ujuzi kuanzia ngazi za chini ambayo itaamua mustakabali wa wanafunzi baada ya kumaliza kiwango fulani cha elimu.

“Kupitia mtaala mpya wa elimu na mafunzo itatakiwa muundo mpya utakaoimarisha upatikanaji wa maarifa, ujuzi na mitazamo itakayozingatia ajira na kujiajiri. Uanzishwaji wa programu utaendana kwa karibu zaidi na mahitaji ya soko la ajira na fursa za kiuchumi nchini,” amesema Prof. Maboko.

Akizungumza katika kongamano hili muhitimu wa Shahada ya Umahili ya Usimamizi wa Miradi, Dkt. Malneste James, ameipongeza serikali kwa kuleta mabadiliko ya sera ya elimu katika wakati muafaka. Hivyo, anategemea maandalizi yanayofanyika kwa ajili ya kuanza kufundisha kupitia sera hii mpya, jamii itashuhudia mabadiliko makubwa.

Kongamano la thelathini na tatu la Wanadhuoni wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania limefanyika Disemba 13, 2023 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambapo wanazuoni wamekutana katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kituo cha mkoa wa Ruvuma na kujadili kuhusu mabadiliko ya sera ya elimu ya mwaka 2014 yanayoanza kutekelezwa hivi karibuni.

Post a Comment

0 Comments