Ticker

6/recent/ticker-posts

TANGA JIJI YAENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA UCHAFU, KUNUNUA VIFAA VYA KISASA KUBEBA TAKA.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imeendelea kutekeleza jukumu la udhibiti taka zinazozalishwa ili zisilete madhara kwa jamii, kwa kuhakikisha magari ya uchukuzi yanaondoa taka na kuzipeleka sehemu maalumu ya kutupia.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira, Kizito Nkwabi amesema kwenye utekelezaji huo halmashauri pia inaendelea kusajili vikundi vya ukusanyaji taka na kubainisha kwamba, "wakati Mwenge wa Uhuru 2023 ulipopita katika Wilaya yetu, moja ya kazi zilizofanywa na Mwenge wa Uhuru, ilikuwa ni pamoja na uzinduzi wa gari jipya la kubeba taka la Halmashauri ya Jiji la Tanga".


Nkwabi amesema gari hilo tayari lipo mtaani likiendelea na kazi hiyo, ikiwa ni moja ya mipango ya halmashauri ya ununuzi wa magari ya kubebea taka ili kurahisisha kazi ya uondoaji wa taka katika mitaa.


Amebainisha kwamba pamoja na ununuzi wa gari hilo, halmashauri inafanya matengenezo ya vifaa na magari mengine ili kuongeza nguvu katika eneo hilo, huku ikijipanga kununua magari ya kisasa zaidi na kuachana na vifaa vilivyopitwa na wakati.


Aidha amefafanua kwamba jiji la Tanga lina kata 27, ambazo kwa pamoja zinazalisha zaidi ya tani 217 za takataka kwa siku,vhasa huzalishwa katika kaya, biashara, viwanda, na mifugo ambapo mbali na jiji kuongeza uw1ezo wake, lakini pia inashirikisha sekta binafsi, na tayari jambo hilo linafanyika katika kata za Nguvumali, Pongwe na Maweni.


"Tayari tunawatambua wadhibiti taka 430, ambao hawa ni wadhibiti taka kwa kutumia mfumo wa urejerezaji taka kuwa mali au kuzirudisha taka kwenye mnyororo wa thamani ili zitumike tena kwa manufaa, na sasa hakuna taka ambayo haiwezi kutumika tena" amesema Nkwabi.


Vilevile amesema kwamba ili kupata mgawanyo mzuri wa gari za kubeba taka, halmashauri imekuwa ikitoa ratiba ya magari ya kubeba taka kwa kila kata, huku akitoa rai kwa wananchi na viongozi katika ngazi husika.


"Niwaombe viongozi na jamii kwa ujumla, kuhakikisha takataka zinawekwa katika vifaa vya kuhifadhia, na watoe taka kwa mujibu wa ratiba ya siku ya kupita gari, lakini pia wasimpe taka mtu asiye rasmi, ambaye hajaidhinishwa na halmashauri kufanya kazi hiyo, mfano unampa taka mtu halafu anaziacha mtaa wa pili, hii sio sawa"


Pamoja na hayo Kizito anakumbushia wajibu wa wakazi kulipa huduma hiyo, 'hii ni sawa na ule usemi wa 'haki huenda na wajibu', watu walipie ada ya huduma hii ambayo kwa kaya ni Tsh. 2000 kwa mwezi, huku maeneo ya biashara yakiwa na viwango vyao kwa mujibu wa ukubwa na aina ya biashara".

Post a Comment

0 Comments