Ticker

6/recent/ticker-posts

KITANDULA - TANESCO ACHENI KUKATA UMEME MPAKANI MWA NCHI KULINDA MAPATO.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko (katikati) akikata utepe ishara ya kuzindua na kuwasha umeme wa REA  katika vijiji vya Magodi na Kigandini wilayani Mkinga.

Na Hamida Kamchalla, MKINGA.


SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO), limetakiwa kuacha kutoa mgao wa umeme katika maeneo yenye vyanzo vikubwa vya mapato hasa mipakani, ili kukwepa kupoteza mapato ya serikali kwa kiasi kikubwa kutoka nchi jirani.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dastan Kitandula wakati wa kuwasha umeme wa REA katika vijiji vya Magodi na Kigandini ambapo amesema mgao wa umeme umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa katika mpaka wa Horohoro wilayani humo.

Kitandula ambaye ni mbunge wa Mkinga amebainisha kwamba serikali inafanya kazi kubwa sana ya kupambana kuhakikisha umeme unapatikana, na kwamba mahitaji yaliyopo ni makubwa kuliko umeme unaozalishwa na kupelekea baadhi ya maeneo kupata umeme mchache.

"Lakini kwa Wilaya ya Mkinga hali ni ngumu, kila siku iendayo kwa Mungu umeme lazima ukatike, tunaelewa wenzetu wanaangalia kwamba kile kidogo wanakipeleka kwenye maeneo ya uzalishaji ili kusikosekane mapato ya serikali, Mkinga hatuna viwanda, kwahiyo ni rahisi sana Tanesco kutuweka pembeni" amesema.

"Lakini wanasahau jambo moja kubwa, Mkinga tuna kiwanda kikubwa kinachotuingizia mapato, ambacho ni ule mpaka (boarder), ile mizigo inayopita pale inatuingizia mapato makubwa sanai, lakini wenzetu wanajisahau kwamba pale panahitaji umeme muda wote,

"Lakini mgao huu wa umeme unaathiri sana kituo chetu, wakati mwengine kwenye kituo cha pamoja Wakenya wanatoka na kulazimika kurudi upande wao ili waweze kufanya kazi, sasa niombe, umeme kwa upande huu wa Mkinga usikatwe kwa sababu tunapoteza mapato" amesisitiza.

Hata hivyo amesema kwamba kero kubwa iliyopo katika Wilaya hiyo ni maji ambayo kwa miaka mingi lakini mbunge huyo aliishukuru serikali kwa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika Wilaya hiyo.

"Tunaishukuru serikali kwa kazi nzuri iliyofanya, lakini zipo kero, tunaishukuru serikali kwa kutuletea mradi mkubwa wa maji kutoka mto Zigi hadi Horohoro wenye thamani zaidi ya sh bilioni 35, tunaomba Mkandarasi yule uendelee kumsimamia kazi ile ikamilike kwa wakati" amesema.

Akizindua kuwashwa kwa umeme huo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Dotto Biteko amesisitiza kero zote zifanyiwe kazi na zitatuliwe kabla Rais Samia Suluhu Hassan hajapita eneo lenye kero hizo na kwamba haitakuwa vema kama kiongozi wa ngazi ya juu akipita akakutana na kero za wananchi.

Baadhi ya wananchi wa vijiji vya Magodi na Kigandini, kata ya Kasera, Wilaya ya Mkinga wameipongeza na kuishukuru serikali kwa kuwapelekea na kuwasambazia umeme kwani ni moja ya kilio chao kikubwa kwa muda mrefu.

"Kabla ya umeme kutufikia tulikuwa na kero nyingi, hospitali wakina mama walikuwa wanajifungua kwa shida, jenereta haikuwa ikikidhi mahitaji hivyo mpaka kusafiri kwenda hospitali ya Wilaya Mkinga" alisema Mwajuma Omari.

Naye Bakari Gaba alisema, "kwa sasa tutafanya jazi zetu vizuri, tumekuwa tukishindwa kuweka hata mashine, sasa tutafungua viwanda na kufanya biashara zetu bila shida, tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuona wananchi wake na kutuletea umeme ".

Post a Comment

0 Comments