Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WA GDSS WAJIZATITI DHIDI YA UKEKETAJI KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

VITUO vya Taarifa na Maarifa Mkoa wa Dar es Salaam vimejipanga kikamilifu katika kukabiliana na vitendo vya ukeketaji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa huo, ambapo imeelezwa yakuwa asilimia 15 ya vitendo hivyo vinafanyika kwenye Mkoa huo hasa katika kata ya Kivule na Kipunguni wilayani Ilala.

Hayo yamebainishwa leo Januari 31,2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) TGNP Mabibo Jijini Dar es Salaam ambapo walikuwa wakijadili Mada isemayo "Takwimu na Athari za Ukeketaji kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Nini Kifanyike?.

Akizungumza na mwandishi wetu, Mdau wa masuala ya Jinsia kutoka Kituo Cha Taarifa na Maarifa, kata ya Kivule Bw.Erick Anderson amesema kuwa athari za vitendo vya ukeketaji hupelekea kupunguza nguvu kazi kutokana na kumwaga damu nyingi wakati akifanyiwa jambo hilo.

Amesema wanawake wanaofanyiwa ukeketaji mara nyingi wanapoteza nguvu ya kujiamini wanapokuwa katika jamii hivyo kudhorotesha uzalishaji mali katika jamii inayowazunguka.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa njia ambayo wamechagua kukomesha ukeketaji kwa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusiana na haki za binadamu, kuifanya jamii itambue madhara ya kitendo hicho cha kikatili pamoja na madhara ya mila potofu.

Kwa Upande wake,Mwanaharakati wa jinsia kutoka kata ya Kipunguni Bi.Fatma Abdulahman amesema wamejipanga vizuri kuwahudumia mabinti ambao watapata taarifa zao kwa kuwahudumia mahitaji msingi kwa kuwawezesha wafikie malengo yao.

Aidha amesema kuwa watoto ambao wamefanyiwa ukeketaji wanawasaidia kisaikolojia  na akiwa si mwanafunzi wanamuwezesha kiuchumi kwa lengo la kumsahaulisha machungu na kumuondoa katika hali ya kujinyanyapaa.

Nae mdau wa GDSS, Bi. Moreen Peter amesema kuanzia hivi sasa atahakikisha anatoa taarifa sehemu husika pindi atakapoona vitendo vya ukeketaji kwenye maeneo ambayo yanamzunguka ili kuokoa jamii ambayo inaangamia kupitia vitendo hivyo.

Semina hiyo ilijikita katika kutambua Takwimu na Athari  za Ukeketaji katika mkoa wa Dar es Salaam na  kuweka suluhisho nini kifanyike kuondoa tatizo hilo ambalo limekithiri nchini kwa kuhatarisha uhai wa watoto wa kike na wanawake.


Post a Comment

0 Comments