Ticker

6/recent/ticker-posts

WATUHUMIWA 335 WANAOJIHUSISHA NA MATUKIO YA KIHALIFU WAKAMATWA MWANZA


Na Sheila Katikula ,Mwanza

Jumla ya watuhumiwa 335 wanaojihusisha na matukio ya kihalifu wamekamatwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mtafungwa wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea hali ya usalama katika mkoa huo.

Amesema watuhumiwa hao 335 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ambapo watuhumiwa 133 wamehojiwa na kufikishwa Mahakamani na watuhumiwa 202 bado wanaendelea kuhojiwa kwani upelelezi utakapo kamilika watafikishwa mahakamani.

Amesema jeshi hilo limefanya misako maeneo mbalimbali na kukamata vitu vikiwemo simu za mkononi zaidi ya 50, dawa za kulevya aina ya mirungi,misokoto ya bangi,vifaa vya kufanyia uhalifu pamoja na vitu vilivyoibiwa sehemu mbalimbali kwenye makazi ya watu.

"Baada ya kuwatia mbaloni washtakiwa wa matukio ya kihalifu waliokamatwa kwenye operesheni hii ya wiki moja tumefanikiwa kuwa kamata watuhumiwa wa vitendo vya uhalifu 47, kuingia nchini bila kibali watano, wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya 51, watuhumiwa wa mauaji 13, watuhumiwa 17 waliojihusisha na kuvunja nyumba na kuiba",amesema Mtafungwa.

"Misako hii ni endelevu kwani tumepata mafanikio ya kuzuia na kudhibiti matukio ya kihalifu kwenye maeneo mbalimbali.

Hata hivyo Kamanda Mtafungwa amewapongeza raia wema waliotoa ushirikiano kwenye operesheni hiyo ya wiki moja na kupelekea kufanikiwa kukamatwa kwa wahalifu hao sanjari na hayo amewataka waendelee kuwa na moyo huwo huwo wa kizalendo ili waweze kutokomeza matukio ya uhalifu kwenye maeneo yao.

Post a Comment

0 Comments