Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KAIRUKI AFUNGUA MAONESHO YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA INDIA

Na Happiness Shayo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amefungua rasmi Maonesho ya pamoja kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na India katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es salaam leo Januari 26,2024, lengo ikiwa ni kuielimisha jamii kuhusu historia na utamaduni uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Ni matarajio yetu kwamba maonesho haya yataongeza ufahamu wa watu kuhusu uhusiano wetu mzuri na kuimarisha urafiki wetu” Mhe. Kairuki amesema.

Mhe. Kairuki amesema kuwa maonesho hayo ya pamoja kati ya Tanzania na India, yanaweka alama muhimu ya uhusiano mzuri na wa muda mrefu baina ya nchi hizo na ni kiashiria cha juhudi za pamoja za muda mrefu katika kujenga diplomasia ya kiutamaduni.

Aidha, amefafanua kuwa kupitia mashirikiano kati ya Tanzania na India, Tanzania imekuwa ikifaidika zaidi kwa kupata fursa za mafunzo kutoka India, na masoko ya mazao yake ya biashara na pia nchi zote mbili zimekuwa zikinufaika kiuchumi, kidiplomasia, kielimu na kiutamaduni.

”Tunaamini mahusiano haya yatafungua fursa zaidi kati ya Tanzania na India na tunaendelea kuona ni namna gani tutashirikiana na kubadilishana utaalamu kati ya nchi zetu mbili katika maeneo ya makumbusho, malikale, utamaduni na mengineyo” amesisitiza Mhe. Kairuki.

Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania wote, raia wa kigeni, hususan kutoka India wenye makazi yao hapa nchi na wanafunzi kutembelea maonesho hayo ili kushuhudia historia ya mahusiano baina ya nchi hizo mbili, masuala ya kifedha na kupata nafasi ya kujifunza mengi kupitia Makumbusho ya Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Balozi wa India nchini Tanzania Manoj Varma ameomba Taasisi ya Makumbusho ya Taifa kulifanya onesho hilo kuwa la kudumu kwa kuzingatia mahusiano ya muda mrefu ya mataifa hayo tangu Karne ya 19 kwenye nyanja za kijamii,kiuchumi na kisiasa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt.Noel Lwoga amesema ufunguzi wa onesho hilo ni mwanzo wa kuanzishwa kwa Makumbusho binafsi ya Taifa la India itakayokua hapa nchini ili kuendelea kurithisha historia ya mahusiano baina ya mataifa hayo mawili kwa vizazi vijavyo.

Maonesho hayo yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya Uhuru wa Taifa la India yamehudhuriwa na raia wa India wanaoishi nchini Tanzania pamoja wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments