Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA UTOAJI CHANJO YA MAGONJWA YA SURUA NA RUBELA, RC TANGA ATAKA ZIANZE NYUMBANI KWAKE.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

ZAIDI ya watoto 318,108 walio chini ya umri wa miaka mitano mkoani Tanga wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubela kupitia kampeni ya Kitaifa kutoka Wizara ya Afya nchini.


Akiongea ofisini kwake, mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema Mkoa huo ni moja kati ya Mikoa inayolengwa na kampeni hiyo ambayo itaanza rasmi februari 15 hadi 18 ikiwa inalenga kutoa chanjo kwa watoto hao.


"Wizara ya Afya na TAMISEMI imepanga kuleta kampeni hii na kama nchi tutaanza kampeni ya chanjo ya surua na rubela na Mkoa wa Tanga ukiwa mmoja wapo baada ya kuripotiwa kuwepo kwa ugonjwa wa surua katika Wilaya 5 mkoani humo,


"Na tumejipangia kutoa chanjo hiyo kwa watoto wasiopungua 318,108, katika maeneo mbalimbali ya halmshauri zetu 11 za Mkoa wetu, kwa maana ya halmashauri zetu 8" amesema Kindamba.


Aidha amebainisha kwamba magonjwa ya surua na rubela husababishwa na virusi ambavyo huenea kwa kasi sana kwa njia ya hewa, hasa pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya.



"Magonjwa haya huathiri watu wa rika zote lakini hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano, hivyo basi wananchi wote wazingatie ushauri wa wataalamu katika kuimarisha afya zetu na masuala ya usafi,


"Kama vile kunawa mikono, kukizuia wakati wa kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakowa, lakini pia kutoa taarifa katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, pale tu itakapoonekana hali siyo ya kawaida ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka" amesisitiza.


Kindamba ameelezea dalili kuu za magonjwa hayo kuwa ni homa, mafua, kikohozi, macho kuwa mekundu na kutoa machozi lakini pia kutokwa na vipele vidogo vidogo katika paji la uso, nyuma ya masikio na hatimaye mwili mzima.


Amesema magonjwa hayo yanasababisha madhara makubwa sana na mbalimbali ikiwemo kutokwa na usaha masikioni ambapo yanaweza kusababisha matatizo ya kutosikia, lakini pia vidonda vya macho ambavyo husababisha kutoona au upofu, kubanwa mbavu na utapiamlo.


"Mgonjwa asipopata tiba sahihi kwa wakati inaweza kupelekea ulemavu na hata kupoteza maisha, magonjwa haya hayana tiba maalumu, hivyo hutolewa kulingana na dalili za madhara ambayo mgonjwa ameyapata,


"Lakini tuna habari njema kwamba magonjwa haya yanazuilika kwa chanjo, na kwa hivyo basi mtoto atapewa dozi za chanjo mara mbili, kwanza anapotimiza umri wa miezi 9 na marudio ni atakapotimiza miezi 18,


"Naomba niwasihi wananchi wote wa Mkoa wa Tanga, wahakikishe watoto wote chini ya umri wa miaka mitano wapelwkwe wakapate chanjo na faida nyingine iliyopo watoto hao watapata chanjo dozi moja na siyo mbili, hii ni kwamaana kwamba ndani ya dozi hiyo kuna mchanganyiko wa dawa za magonjwa yote" amefafanua.


Hata hivyo Kindamba amewatoa wasiwasi wananchi kwamba chanjo hizo ni salama na hazina madhara yoyote wala athari kwa watoto, lakini pia alielekeza maeneo ambayo wataalamu watapata watoto hao kwa wingi wake kuwa ni mashuleni.


"Najua panaweza pakatokea kurupushani za hapa na pale lakini niwatoe hofu kwamba chanjo hizi ni salama, na nimewaelekeza wataalamu wangu wa afya waanze kuchanja nyumbani kwangu na viongozi wangu, hii yote ni kuwathibitishia kuwa ni salama" amesema.

Post a Comment

0 Comments