Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. MPANGO HARAKISHENI USANIFU BARABARA YA OLD KOROGWE - MABOKWENI KM 127

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta, Philip Isdor Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi kuharakisha usanifu wa barabara ya Old Korogwe -Magoma - Kwa Mndolwa- Bombomtoni- Maramba-Mabokweni KM 127, ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami na hivyo kuibua fursa za uzalishaji na kiuchumi kwa wakazi wa Wilaya za Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga naTanga.

Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Tanga Dkt. Mpango amezungumzia umuhimu wa wakazi wa mkoa huo kupanda miti kwa wingi na kuitunza ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoathiri miundombinu ya barabara na madaraja kwa kiwango kikubwa.

"Pandeni miti ya kivuli na matunda kwa wingi ili kulinda uoto wa asili na hivyo kulinda barabara na madaraja yanayojengwa kwa fedha nyingi za Serikali", amesema Dakta, Mpango.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo utakamilika ifikapo mwezi Machi mwaka huu na tayari Wizara imeiweka barabara hiyo kwenye mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami katika bajeti ijayo.

Naibu Waziri Kasekenya amesema barabara hiyo ambayo pia ni ya kimkakati inayopita maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na matunda pia inapita mpakani hivyo ikikamilika itachochea ukuaji wa kichumi kwa wakazi wa mkoa wa Tanga na kuchochea biashara na utalii kati ya Tanzania na Kenya.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya akifafanua jambo katika ziara ya Makamu wa Rais  Mkinga mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya akiteta jambo na Naibu Waziri TAMISEMI mhe. Deogratius Ndejembi na Naibu Waziri Maliasili na Utalii mhe. Danstan Kitandula katika ziara ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango wilayani Mkinga mkoani Tanga.

Post a Comment

0 Comments