Ticker

6/recent/ticker-posts

ELIMU YA BRELA YAWAFIKIA VIZIWI KONDOA


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa elimu kuhusu huduma za Taasisi kwa watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), walaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Elimu hiyo imetolewa leo Februari 6, 2024 lengo likiwa ni kuhamasisha kundi hilo muhimu ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA.


Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Leseni kutoka BRELA Bi. Winfrida Gaudence amesema kuwa Taasisi imeitikia ombi la Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) la kuwapatia elimu hiyo ambayo ni yenye manufaa kwa biashara zao.



Ameeleza kuwa faida za kurasimisha biashara BRELA ni pamoja na kuwa na upekee katika soko, kunufaika pale wanapohitaji mikopo katika taasisi za kifedha, kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa za ukuzaji wa biashara.

" Niwapongeze kwa mwitikio wenu na tumefurahi kujumuika nanyi Ili kuwapatia elimu hii ya urasimishaji wa biashara na ninaamini mtakwenda kuitumia vema na kwakuwa tumefika hapa, kwa wale wenye uhitaji wa usaidizi katika Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS), tupo kufanikisha hilo," ameongeza Bi. Gaudence.

Sambamba na hilo amewaomba wenye vikundi vya kibiashara kusajili majina yao ya biashara au kampuni na kupata Leseni ili iwe rahisi kufanya biashara kwa uhuru zaidi.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TAMAVITA Bw. Kelvin Nyema ameipongeza BRELA kwa kufika wilayani Kondoa na kukutana na watu wenye ulemavu wa kusikia na kuwapatia elimu ambayo itawasaidia kujikwamua na kusonga mbele zaidi kwenye biashara zao.


" Naomba kwanza niwaombe mumfikishie salamu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA kuwa tunashukuru sana kwa kufadhili na kufanikisha mafunzo haya, niwahikikishie watu wenye ulemavu wa kusikia kuwa elimu waliyoipata leo itafungua fursa zaidi kwani kuna wafanyabiashara, wakulima na hata wajasiriamali ambao waliihitaji sana elimu hii," ameongeza Bw. Nyema


Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofadhiliwa na BRELA yamewakutanisha viziwi zaidi ya 50 ambao kwa umoja wao wamesema wamehamasika na watakuwa mabalozi wa huduma za BRELA.


Post a Comment

0 Comments