Na. Zainab Ally - Songea.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Thomas amewahimiza Watanzania na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo ya Malikale ambazo zimetunza historia maridhawa ya nchi yetu,
Aliyasema hayo leo tarehe 27.02.2024 katika Kilele cha Tamasha la Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji linalofanyika kila mwaka katika Viwanja vya Mashujaa mjini Songea mkoani Ruvuma.
Akiwa katika Tamasha hilo Mhe. Laban alisema, "Sera ya Malikale ya Mwaka 2008 inaruhusu uwekezaji katika maeneo ya kihistoria ya Malikale lakini bado mwitikio wa uwekezaji kwa watanzania ni mdogo, hivyo niwasihi watanzania wenzangu kuchangamkia fursa hiyo."
Aidha, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambao ni wasimamizi wa Vituo 5 vya Malikale ambazo ni Isimila, Kalenga, Caravan Serai, Dkt. Livingston na Nyumba ya Kumbukizi ya Mwl. Nyerere wameshiriki Tamasha hilo kwa kunadi malikale zake na vivutio vingine vya utalii na fursa za uwekezaji katika maeneo hayo ambayo ni hazina kwa Taifa.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba alisema, "Tamasha hili hutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uhifadhi wa Malikale hizi, kuenzi na kuendeleza uzalendo, amani na mshikamano, vitu ambavyo ni urithi wetu kutoka kwa mashujaa wa Vita vya Majimaji."
Vilevile, Kamishna Wakulyamba aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake ikiwemo TANAPA wamepewa dhamana ya kuyalinda na kuyatunza maeneo haya kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho, hivyo ushiriki wa taasisi hizi ni kutoa fursa kwa watanzania na wageni kutoka mataifa ya nje kujifunza, kuzielewa na kuzitembelea.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - Kevin Nkulila akimaribisha mgeni rasmi na jopo lake katika banda la TANAPA alisema, "Licha ya Shirika letu kuwa na Hifadhi za Taifa 21 pia tuna vituo vya Malikale 5 ambapo malikale moja ya Kalenga ina historia inayokaribiana sana na hii ya vita vya Majimaji. Vita ya Majimaji ilipiganwa kupinga utawala wa Kijerumani halikadhalika Chifu Mkwawa alipinga utawala wa Kijerumani huko Iringa, hivyo tuko hapa kunadi historia ya shujaa huyu na maeneo mengine yenye historia tofauti na vivutio vingine vya utalii.
"Hata hivyo, kutokana na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na mataifa yaliyoko Kusini mwa Afrika, Tamasha hili la Kumbukizi ya vita ya Majimaji limekuwa likihudhuliwa na wenzetu kutoka Malawi, Zambia na Afrika ya Kusini, hivyo ushiriki wa TANAPA pia ni kupata fursa ya kuwavutia wananchi wa mataifa hayo kuja kuwekeza na kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania ambavyo ni miongoni mwa vivutio bora barani Afrika na Dunia kwa ujumla", aliongeza Kamishna Nkulila.
TANAPA ni miongoni mwa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambao hushiriki kila mwaka kuadhimisha Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji kwa kunadi vivutio vyake na fursa za uwekezaji ili kupata watalii wengi zaidi.
0 Comments