Ticker

6/recent/ticker-posts

MBETO AFANYA ZOEZI LA KUSIKILIZA MAONI YA WANANCHI Z'BAR.

NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amezitaka taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza utamaduni wa kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili Wananchi.

Akizungumza katika zoezi la kupokea na kusikiliza changamoto za wananchi, lililofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar,amesema utaratibu huo utakuwa endelevu hadi ngazi za shehia mbali mbali mijini na vijijini.

Alibainisha kuwa kuna baadhi ya sekta za umma na ndani ya Chama Cha Mapinduzi watendaji wake wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao na kusababisha Wananchi kuilamu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika maelezo yake,Katibu huyo wa NEC Mbeto,alieleza kuwa lengo la kufanya zoezi hilo ni kubaini na kuratibu changamoto na maoni ya Wananchi ili zitatuliwe kwa wakati na taasisi husika.

"Katika jamii zetu kuna malalamiko ya migogoro ya muda mrefu mwingine inaweza kutatuliwa na ngazi za shehia,wilaya,idara na wizara lakini bado kuna baadhi ya wananchi hawati hata haki ya kusikilizwa"alisema Mbeto.

Alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni mali ya Wananchi wote kwani ndio waliotoa ridhaa ya kuziweka madarakani Serikali zote mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivyo wana haki ya kusikilizwa.

Wakizungumza baadhi ya Wananchi waliofika katika Ofisi hiyo kuwasilisha changamoto zao,wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi na kueleza kuridhishwa kwao na utaratibu huo unaolenga kumaliza kero na changamoto za wananchi.

Kwa upande wake Kassim Issa Abdulla mkaazi wa shehia ya Magomeni Zanzibar,alisema CCM imeamua kuleta mabadiliko makubwa hasa katika kuwasaidia Wananchi wa tabaka la chini kupata ufumbuzi wa changamoto zao.

"Nimefika hapa Ofisini kuwasilisha changamoto yangu ambayo ni kuhusu madai yangu ya kutapeliwa ardhi nashukru suala hilo limefikishwa taasisi husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi",alisema Kassim.

Naye Mkaazi wa Fuoni Zanzibar Zuhura Hassan Mjaka,alishauri utaratibu huo kuwa endelevu kwani wananchi wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na kukosa sehemu sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akipokea na kusikiliza maoni na changamoto za wananchi huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments