Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO ASISITIZA USAFI WA MAZINGIRA KWA WAWEKEZAJI KWENYE FUKWE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahimzia wawekezaji wanaowekeza katika fukwe mbalimbali nchini kuhakikisha zinakuwa safi ili kutunza mazingira.

Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na kituo cha Radio cha TBC Taifa leo tarehe 19 Februari, 2024. 

Amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya uchafu katika fukwe nyingi nchini hususan chupa za plastiki zilizotumika ambazo si tu husababisha uchafu wa mazingira lakini pia ni kero kwa wageni wanaozitembelea.

Kutokana na hali amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa ambako fukwe hizo zinapatikana, licha ya shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira wanazotekeleza pia zisimamie shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo hayo.

Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa halmashauri hizo ziwe na mpango wa kushirikiana na vijana wanaojitolea kuikota chupa zinazotupwa katika fukwe kwa kuwapa motisha hivyo maeneo hayo kuendelea kuwa safi.

Pamoja na kutoa pongezi kwa viwanda vinavyorejeleza chupa za plastiki amewahimiza wenye viwanda wengine kuchukua hatua hiyo ambayo itasaidia katika kuondosha taka za chupa katika fukwe. 

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inashirikiana bega kwa bega na wadau mbalimbali kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mazingira kwenye fukwe nchini zinakuwa safi.

Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Jafo amewataka wenye magari kuwa na vyombo maalumu vya kuhifadhia taka badala ya kutupa ovyo njiani ili kutunza mazingira ya barabarani.  

“Tuna kazi kubwa ya kutengeneza ustaarabu, utakuta mtu akiwa kweny basi anakunywa maji anatupa chupa nje na inazagaa ovyo na kuchafya mazingira hivyo tunawataka wenye magari na wenye mabasi wote kuwa ‘dustbin‘ kwa ajili ya kuwekea taka na wenye magari simamieni zoezi hilo,“ amesisitiza Dkt. Jafo.

Ikumbukwe kuwa awali kulikuwepo na changamoto ya chupa za plastiki ambazo hutupwa ovyo na sasa hivi zimekuwa ni malighafi kwa viwanda kwa ajili ya kurejelezwa.

Kutokana na hatua hiyo Serikali imekuwa ikihamasisha viwanda kufanya urejelezaji wa chupa za plastiki ambazo huokotwa na kukusanywa katika maeneo mbalimbali yakiwemo fukwe.


Post a Comment

0 Comments