Ticker

6/recent/ticker-posts

CDF, CLIW WAZINDUA MRADI MPYA WA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI YA VVU WILAYANI KINONDONI.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Shirika la Community Led Initiative for Women (CLIW) wamezindua mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni, ukiwa na lengo la kuchangia juhudu za serikali katika kutekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuharakisha hatua na Uwekezaji kwa Afya na Ustawi wa Vijana 2021/22 - 2024/25 (NAIA-AHW).

Mradi huo utachangia afua kuu Nne kati ya afua sita ikiwemo Kuzuia VVU, Kuzuia mimba za Ujana, Kuzuia Ukatili wa Kijinsia, Kimwili na Kihisia, Kuboresha Lishe, Kukuza Ujuzi na kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana wanaoishia na virusi vya ukimwi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 14, 2024 wakati wa uzinduzi wa mradi huo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji, Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti amesema mradi huo utachangia dhamira ya Tanzania katika utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu VVU na UKIMWI la mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu na Agenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063, ili kuwezesha Tanzania kufanikisha malengo kwa mujibu wa taratibu na kanuni bora za kitaifa na Kimataifa.

"Tanzania imelenga kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kitaifa la 95-95-95 (Asilimia 95 ya wanaoishi na VVU watambue hali zao, asilimia 95 ya WAVIU wawe wameanza dawa za kupunguza makali ya VVU na asilimia 95 ya walioanza dawa wapunguzwe kiwango cha virusimwilini) ifikapo mwaka 2030". Amesema Mtengeti.

Aidha amesema lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake vijana, hasa wale walio katika mazingira hatarishi kama vile wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au wanaofanya kazi katika mazingira yenye hatari ya kuambukizwa VVU, wanapata uelewa na ujuzi wa kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU.

"Kupitia mradi huu, tunalenga kuhamasisha upimaji wa VVU, upatikanaji wa huduma za afya bora na salama, na matumizi sahihi ya dawa za kujilinda na kupunguza makali ya VVU". Ameeleza Mtengeti.

Pamoja na hayo amesema kwa kufanikisha malengo ya mradi huo, CDF na CLIW watatekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa vijana hao juu ya kujitambua, kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU, ushauri nasaha, upimaji, na matumizi sahihi ya dawa za kujilinda na kupunguza makali ya VVU.

"Vijana hawa watapewa ujuzi na kisha kufanya kazi ya kuelimisha wenzao katika jamii kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mijadala, midahalo na vipeperushi vyenye jumbe mbalimbali". Amesema

Amesema kuwa kupitia mradi huo, wahudumu wa afya watapatiwa mafunzo na ujuzi wa kutoa huduma bora na rafiki kwa wasichana na wanawake vijana wanaoishi au walio hatarini kupata maambukizi ya VVU ili kupunguza maambukizi ya VVU.

"Tunaamini kuwa mradi huu utachangia kujenga uelewa zaidi miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na kutafuta huduma za afya bora. Tunatoa wito kwa jamii na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo ya mradi huu muhimu". Ameongeza Mtengeti

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Kinondoni, Ezra Ngereza amewataka wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu mashuleni na vyuoni ili kuepusha mmomonyoko wa maadili kwa vijana na wanawake.

"Ikiwa kijana hataandaliwa vizuri namna ya kuhimili na kujitawala lakini pia kujikinga na watu wabaya lazima mimba za utotoni zinaendelea kuwepo, matukio ya ukatili yataendelea na uonevu kuwa mwingi"

"Miradi kama hiyo ipo lakini bado haitoshi, kwasababu Kinondoni ni Moja ya Manispaa yenye wakazi wengi ambao ni takribani Milioni 1 kwa mujibu wa senza iliyopita na ndiyo Dar es Salaam na Tanzania kwasababu vyuo vingi elimu ya juu viko hapa, na tuna vijana wengi sana wanaotoka mikoani kuja kusoma hapa, maisha ya mkoani na maisha ya Dar es Salaam ni tofauti, wasipoandaliwa vijana hasa wakike kukabili changamoto wanaweza wakajikuta wanapata vishawishi na madhara". Amesema 
 Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Kinondoni, Ezra Ngereza akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni, ukiwa na lengo la kuchangia juhudu za serikali katika kutekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuharakisha hatua na Uwekezaji kwa Afya na Ustawi wa Vijana 2021/22 - 2024/25 (NAIA-AHW). Hafla hiyo imefanyika katika ofisi ya Mgnga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo Machi 14, 2024 Jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Kinondoni, Ezra Ngereza akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni, ukiwa na lengo la kuchangia juhudu za serikali katika kutekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuharakisha hatua na Uwekezaji kwa Afya na Ustawi wa Vijana 2021/22 - 2024/25 (NAIA-AHW). Hafla hiyo imefanyika katika ofisi ya Mgnga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo Machi 14, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji, Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni, ukiwa na lengo la kuchangia juhudu za serikali katika kutekeleza Ajenda ya Kitaifa ya Kuharakisha hatua na Uwekezaji kwa Afya na Ustawi wa Vijana 2021/22 - 2024/25 (NAIA-AHW). Hafla hiyo imefanyika katika ofisi ya Mgnga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo Machi 14, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments