Ticker

6/recent/ticker-posts

HAKUNA MWANAFUNZI ATAKAYESHINDWA KUJIUNGA SEKONDARI KWA SABABU WA UFINYU WA MIUNDOMBINU 2028

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema hakuna mwanafunzi atakayeshindwa kujiunga na sekondari kwa sababu ya ufinyu wa miundombinu ifikapo mwaka 2028 kwakuwa imeshafanya maandalizi ya kupokea  wanafunzi wa mikondo  miwili  ambao watamalizia  elimu ya msingi mwaka 2027.

Wanafunzi hao ambao ni wale wanaotarajia kumaliza elimu ya msingi kupitia mtaala mpya ambao wataishia darasa la sita pamoja na watakaomalizia darasa la saba mwaka huo ambao kwa  sasa wapo darasa la nne.

Akizungumza katika kikao kazi na wahariri pamoja na Waziri wa Elimu Profesa Adolph Mkenda, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Atupele Mwambene alisema miongoni mwa vitu ambavyo wamezingatia wakati wakutekeleza muongozo  mpya wa utoaji elimu ni  kuandaa miundombinu ya msingi ambayo itawezesha kutekeleza mwongozo huo.

“Kama mnavyoona  utekelezaji wa sera  hii ya elimu  kwa upande wa  umalizaji wa elimu ya msingi inaenda mpaka 2028 ndo wanafunzi wanaanza kuishia darasa la sita lakini wakati  huo huo kutakuwa na wale wa darasa la saba nao watakuwa wanamaliza.

“Lengo lakuweka utekelezaji huu mwaka 2028 ni pamoja na kutoa muda  kwa serikali kuandaa  miundombinu ya msingi ikiwemo madarasa,walimu,vitabu hivyo ifikapo muda huo hakuna mwanafunzi ambaye atashindwa kuendelea  na masomo,”alisema Mwambene.

Alisema wanafunzi hao watakaoanza kidato cha kwanza wataanza na mitaala ya mafunzo ya amali  pamoja na jumla.

“Wanafunzi watakaofundisha masomo ya jumla watajikita zaidi katika mambo ya kitaaluma huku wale watakaofundishwa  masomo ya amali  watasoma zaidi mambo ya ujuzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne,”alisema Mwambene.

Kwa upande wa Profesa Mkenda akifungua mafunzo hayo alisema serikali imejipanfa vizuri hasa katika mitaala ya mafunzo ya amali ambapo kabla ya utekelezaji wake wameenda katika nchi tofauti tofauti wanazofanya mambo hayo kuchukua ujuzi.

“Huu mtaala wa mafunzo ya amali ni hiyari,hakuna mtu atakayelazimisha,kabla ya mwanafunzi kupelekwa kutakuwa na makubaliano baina ya mzazi na wanafunzi  na walimu,lengo letu watu wamalize elimu ya msingi wakuwa na ujuzi,”alisema Profesa Mkenda.

Alisema  serikali imeshafanya uchunguzi na kujiridhisha shule zote ambazo zinataka kutoa mafunzo ya amali kama zinakidhi vigezo vinavyohitajika kutoa elimu hiyo.

“Kulingana na vigezo tulivyoviweka shule 96 zimepitishwa  kufundisha masomo ya amali Tanzania Bara,kati ya hizo 28 ni za serikali  na 68 ni za binafsi,”alisema Profesa Mkenda.
Post a Comment

0 Comments