Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda amewaomba wadau wote kuendeleza ushirikiano na Baraza la Ushindani ( FCT) katika kuongeza uzoefu, ufanisi katika majukumu mbalimbali.
Hayo ameyasema wakati akifunga semina hiyo Aprili 15 2024 Mkoa wa Mwanza, Machunda, amesema semina hiyo ni muhimu hivyo elimu walioipata itawasaidia kutambua haki na kujua wajibu wao.
Amesema ili kusimamisha ushindani wa haki na kumlinda mlaji kwani Sheria zinataka kuwepo na ushindani wa haki na kumlinda mlaji.
"Wadau wamepata fursa ya kutoa ushauri kuboresha mawasiliano na Baraza hili katika masuala mbalimbali na leo ni sehemu ya wao kutatua changamoto mbalimbali za ushindani wa biashara na udhibiti wa soko,"amesema Machunda.
Aidha ametoa shukurani kwa baraza hilo na Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya semina mkoani humo na kuwapatia elimu wadau.
Akizungumza Kaimu Msajili na Mkuu wa FCT, Kunda Mkenda wakati wa semina ya siku moja kwa wadau mbalimbali iliofanyika mkoani Mwanza amesema Baraza limesajili jumla ya mashauri 442 kati ya hayo 429 yameishwa sikilizwa na kutolewa maamuzi na baraza hilo katika kipindi cha mwaka 2007 hadi Machi 2024.
Amesema Baraza limefanikiwa kushughulikia mashauri yalioletwa mbele yake kwa asilimia 97.1 huku mashauri 13 yaliobaki yapo kwenye hatua mbalimbali za usikilizwaji.
"Baraza hili limeanzishwa chini ya kifungu cha 83(1), cha Sheria ya Ushindani Na.8 ya mwaka 2003 inayolenga kukuza na kulinda ushindani wa kibiashara na kumlinda mlaji dhidi ya matokeo ya ukiritimba na tabia potofu katika soko,"amesema Mkenda.
Amesema kutokana na changamoto zilizojitokeza za watu wengi kutolijua baraza hilo kwa mara ya kwanza wameamua kufanya semina hiyo kwa wadau mbalimbali mkoani humo ili waweze kujua haki zao, umuhimu wa baraza na kazi zake.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa semina hiyo akiwemo Zahara Magambo, ameeleza kuwa kupitia semina hiyo ameweza kufahamu sehemu ya kupata haki zake endapo atakuwa ajaridhishwa na maamuzi yaliotolewa aidha na Tume ya Ushindani(FCC), EWURA, TCRA, TCAA, LATRA na PURA.
"Sijawai kupata changamoto lakini semina hii imenifumbua macho ikitokea nikipata changamoto najua naanzia wapi," ameeleza Zahara.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa wajasiriamali wabunifu Tanzania,Fabiani Semba ameeleza kuwa kupitia semina hiyo ameweza kufahamu wapi pa kwenda kwani katika sekta ya mawasiliano kumekuwa na mambo mengi yakitokea huku wakiwa hawajui wapi pa kwenda kutoa malalamiko.
"Niko tayari kutumia Baraza kama sehemu ya kupata msaada na suluhisho kwani itasaidia kukua kiuchumi hivyo elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili kulifahamu Baraza hilo na kazi zake na kutofautisha na Tume ya Ushindani ili waweze kupata haki zao,"amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo(TCCIA),Mkoa wa Mwanza Gabriel Kenene, ameeleza kuwa amejifunza namna ambavyo rufaa zinavyopatikana na kutolewa.
"Nimejifunza kwamba mamlaka hizi za udhibiti ikiwemo EWURA pale inapotokea mtu hajaelewa au utata umetolewa aende wapi,kumbe kuna chombo ambacho unaweza kukata rufaa na kinaondoa utata huo,kinachofurahisha rufaa zinachukua muda mfupi kwani wafanyabiashara hawapendi usumbufu wa kitu kinachochukua muda mrefu hivyo anaona ni bora haki yake ipotee kwa sababu ya muda.
"Nitoe wito kwa wafanyabiashara wanapoona hawajatendewa haki na mamlaka hizi kama LATRA ni vizuri wakafuate haki yao kupitia Baraza hilo kwani gharama zao ni ndogo, nitakuwa balozi kwa kuhakikisha elimu hii nitaipelekwa kwa wadau ambao wanaweza kukutana na kadhia," amefafanua.
0 Comments