Ticker

6/recent/ticker-posts

MADEREVA BODABODA MUHEZA WAFURAHIA ELIMU YA USALAMA BARABARANI,WAKIRI KUWA CHANZO CHA AJALI


Na Mwandishi Wetu,Muheza

ELIMU ya Usalama barabarani inayotolewa na Shirika la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania imewafikia madereva bodaboda wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia bodaboda walioko katika Wilaya zote za mkoa huo.

Kwa mujibu wa Amend ni kwamba baada ya elimu hiyo kutolewa katika Jiji la Dodoma,mradi huo wa elimu ya Usalama barabarani kwa bodaboda ulianza katika Jiji la Tanga na sasa wameamua elimu hiyo itolewe katika Wilaya zote za Mkoa huo na leo imewafikia bodaboda wa Wilaya ya Muheza.

Wakizungumza leo Aprili 7,2024 wakati wa utolewaji wa elimu hiyo ya usalama barabarani, madereva bodaboda wamekiri kukosekana kwa elimu hiyo imesababisha wengi wao kuwa chanzo cha ajali za barabara,hivyo elimu hiyo imekuja wakati muafaka.

Wakieleza zaidi madereva hao wa eneo la Mkanyageni barabara kuu ya Tanga Segera wamesema wanaushukuru Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, Amend pamoja na Kikosi cha Usalama barabarani kwa kuwapatia mafunzo hayo ya usalama barabarani

Wamesema kupitia elimu hiyo sasa watakuwa wakizingatia Sheria za usalama barabarani na hivyo kujiepusha na ajali zinazotokana na kutofuata sheria huku wakifafanua baadhi ya madereva bodaboda wamejifunzia mtaani na hivyo kutokuwa na elimu inayowawezesha kuwa makini.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo dereva bodaboda Shaban Shekiondo amesema kwamba wanaushukuru kwa kampeni hiyo na kwamba wanaamini watakuwa na uwezo wa kutii sheria za usalama barabarani.

"Tumekuwa tukitoa huduma ya kusafirisha abira kwa kutumia bodaboda lakini wengi wao hawana elimu ya usalama barabarani na hivyo matukio ya ajali yamekuwa mengi na kusababisha ulemavu na vifo kwa baadhi yao."

Ameongeza elimu hiyo imewaongezea uelewa kuhusu usalama barabarani wanapokuwa barabarani.

Kwa upande wake dereva bodaboda Meshark Mhando amesema kuwa kupitia elimu ya usalama barabarani iliyotolewa na Kikosi cha Usalama barabarani Wilaya ya Muheza pamoja na Maofisa wa Amend ni matarajio yao wanakwenda kupunguza ajali sambamba na kufuata sheria kikamilifu.

Awali Kaimu Mkuu wa usalama barabara Wilaya ya Muheza DTO Herberth Kazonde amesema kwamba kupitia ufadhili wa ubalozi wa Uswizi nchini Tanzania ,Amend wamekuwa wakifanikisha mafunzo hayo kwa kushirikiana na wadau muhimu kama Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama barabarani.

"Kupitia shirika la Amend elimu tunatoa elimu hii kwa madereva bodaboda na tunaamini itawasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali sambamba na makosa mbalimbali ya barabara ambayo yangeweza kuzuilika."

Ameongeza kuwa kampeni hiyo tayari imeanza kuleta matunda katika maeneo ambayo elimu imeshafika kwani makosa ya barabara yameweza kupungua kwa kiwango cha kuridhisha.

"Hivyo tunawashukuru ubalozi wa Uswizi kwa kuja na mradi huu wa elimu ya usalama kwa kundi hili la bodaboda ndani ya Wilaya zetu na Mkoa wetu."

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo kutoka shirika la Amend Ramadhani Nyaza amefafanua kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliona wapeleke kampeni hiyo katika eneo la Mkanyageni kwani limeoneka ni hatarishi kwa ajali za barabara.

Amesema kwamba "Tumekuja kutoa elimu ya usalama barabara, tumewafundisha umuhimu wa wao kuhakikisha wanakuwa salama muda wote wanapotumia vyombo vya moto."

Post a Comment

0 Comments