Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI PINDA AKABIDHI GARI LA WAGONJWA MPIMBWE

Na Munir Shemweta, MLELE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Mhe, Geophrey Pinda amekabidhi gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibaoni.

Mhe, Pinda amekabidhi gari hiyo tarehe 4 Mei 2024 katika hafla maalum iliyofanyika eneo la Kibaoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Mlele akiwemo Mkuu wa wilaya hiyo Alhaji Majid Mwanga na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud.

Kukabidhiwa kwa gari hilo kunaifanya halmashauri ya Mpimbwe kuwa na jumla ya magari matatu ya kubebea wagonjwa yanayohudumia vituo vya afya vya Kibaoni na Usevya huku gari moja ikihudumia hospitali ya wilaya ya Tupindo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Pinda amewaomba wananchi wa kibaoni kuitumia gari hiyo kwa manufaa yao huku akimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe kuhakikisha gari waliyokabidhiwa inabakia kwa matumizi ya kituo hicho cha afya cha Kibaoni.

‘’Gari ya Kibaoni ikae kibaoni na kule Mamba nikuombe vile vile apatikani dereva haraka na akae pale gari inapolala kwa sababu magari haya siyo mapambo na ni huduma muhimu kwa wananchi’’ alisema Mhe, Pinda

Ameweka wazi kuwa, gari hilo linaenda kuongeza uwezo kwa kituo hicho cha afya kwa kuwa mtu akipata rufaa kutoka Kibaoni kwenda Hospitali ya wilaya mafuta hayatatumika sana tofauti na hapo awali ambapo ililazimika mgonjwa kupelekwa sumbawanga.

Upatikanaji gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Kibaoni kutasaidia kutatua changamoto za usafiri sambamba na kurahisisha huduma za dharura kwa maeneo jirani na hiyo inatokana na kuongezeka kwa mahitaji katika eneo la Kibaoni kama vile uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda.

Mhe, Pinda amewaeleza wananchi wa Kibaoni kuwa, gari iliyokabidhiwa ni mali yao na itatumika kwa kazi za dharura hasa wagonjwa na sasa hakutakuwa tena na ulazima wa kukodi bajaji kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa walio katika hali hatarishi na atabebwa na gari hiyo ku[elekwa mahali ambapo madaktari wamependekeza kupelekwa.

Wananchi wa Kibaoni wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda kwa kusaidia upatikanaji wa gari hilo la wagonjwa pamoja na fedha za ujenzi wa kituo cha afya cha Kibaoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya halmashauri ya Mpimbwe, mwezi Januari 2024 kituo hicho kilipokea shilingi milioni 175 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na umaliziaji majengo ya Maabara, Jengo la Mama na Mtoto, Upasuaji na Kichomea Taka.

Ukamilishaji wa kituo cha Afya Kibaoni utatoa huduma kwa wananchi takriban 28,817 wa kata ya kibaoni na viunga vyake.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akikata utepe kuzindua gari la kubebea wagonjwa la Kituo cha afya cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akimkabidhi fungua ya gari la wagonjwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi Shamim Daudi tarehe 4 Mei 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Myumba na Maendeleo Mhe Geophrey Pinda (katikati), Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga (aliyevaa tai), Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud (aliyenyoosha funguo) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe Silas Ilumba (kushoto) wakifurahia mara baada ya makabidhiano ya  gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa Kibaoni mara baada ya kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha afya kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akiwaongoza viongozi wengine kwenda kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.

Post a Comment

0 Comments