Ticker

6/recent/ticker-posts

PURA, India wateta duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta, gesi asilia

Ubalozi wa India Nchini Tanzania umekutana na kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kupata taarifa zaidi kuhusu zoezi la kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia linalotarajiwa kufanyika Tanzania Bara Mwaka huu.

Mazungumzo hayo yamefanyika Mei 14, 2024 katika Ofisi za PURA - Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu wa Pili wa Balozi wa India Nchini Tanzania (Masuala ya Biashara) Bw. Narender Kumar na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Danstan Asanga.

Akizungumza katika kikao kati ya pande hizo, Bw. Kumar alieleza kuwa, mara baada ya kusikia mpango wa Serikali wa kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia kupitia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2024/25, Ubalozi wa India Nchini Tanzania uliona vyema kukutana na Mamlaka husika kufahamu kwa mapana kuhusu suala hilo ili waweze kutoa taarifa kamili kwa kampuni na wadau nchini India.

"Ni matumaini yetu kuwa kampuni kutoka nchini India zitavutiwa na taarifa hii ndio sababu tumeamua kutafuta taarifa zaidi zitakazowasaidia katika kufanya maamuzi kushiriki katika zoezi la kunadi vitalu na hatimaye kuwekeza katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini Tanzania" aliongeza Bw. Kumar

Akitoa maelezo kuhusu duru ya tano ya kunadi vitalu, Mha. Asanga alieleza kuwa PURA, kwa niaba ya Serikali, imeendelea na maandalizi ya zoezi hilo na kwamba tayari kazi mbalimbali zimekamilika ikiwemo maandalizi ya Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji wa Mapato ambao umewasilishwa Wizara ya Nishati kwa hatua zaidi.

Kazi zingine ni pamoja na uwekaji wa mipaka ya vitalu vitakavyoingizwa katika mnada mara baada ya kupata ridhaa ya Wizara ya Nishati na maandalizi ya vifurushi vya data za petroli.

Vile vile, Mha. Asanga alieleza kuwa mapitio ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 yanaendelea ili kuangalia vifungu vya Sheria vinavyohitaji maboresho. PURA inashiriki kwenye mapitio haya.

Kuhusu lini zoezi hili litafanyika, Mha. Asanga alibainisha kuwa kazi ya kunadi vitalu itafanyika mapema mara baada ya kukamilika kwa maandalizi ya msingi ikiwemo mapitio ya Sheria ya Petroli 2015 na kuwa mpango wa serikali ni kuzindua duru hiyo mwaka huu.

Mbali na kujadili duru ya tano ya kunadi vitalu, Ubalozi wa India Nchini Tanzania na PURA zimejadili pia uwezekano wa kuanzisha mashirikiano baina ya mamlaka za udhibiti wa utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania na India.

Pande hizo pia zilijadili uwezekano wa kushirikiana katika programu za kujenga uwezo kwa watumishi katika masuala ya mafuta na gesi asilia kupitia ufadhili wa Serikali ya India.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mha. Danstan Asanga (wanne kushoto) akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya PURA na Ujumbe wa Ubalozi wa India Nchini Tanzania ukiongozwa na Katibu wa Pili wa Balozi wa India Nchini Tanzania Bw. Narender Kumar (wapili kulia)
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mha. Danstan Asanga (wakwanza kulia) akitoa maelezo wakati kikao kati ya PURA na Ujumbe wa Ubalozi wa India Nchini Tanzania ukiongozwa na Katibu wa Pili wa Balozi wa India Nchini Tanzania Bw. Narender Kumar (wakwanza kushoto)

Post a Comment

0 Comments