NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WATAALAMU kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) pamoja na Wataalamu kutoka Wakala wa Karakana Kuu ya kutengeneza Magari Zanzibar (GAWS) wamekutana kujadili namna watakavyobadilishana uwezo kuhakikisha taasisi hizo zinafanya vizuri katika utoaji huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14,2024 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji GAWS Ndg. Hussein Abdi Hussein amesema wamekutana kutimiza agizo la serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuunda ratiba ya pamoja ambayo itatumika kuweka kumbukumbu za ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali.
Amesema ratiba hiyo itawasaidia kufanya tathimini kuona mambo waliyofanikiwa kuyafanya baada ya ratiba hiyo kukamilika na kubaini vikwazo mbalimbali ili kuboresha huduma.
"Tumeshaweka makubaliano , tumekutana jana na leo katika kutengeneza ratiba ya utekelezaji wa hayo makubaliano ambayo tayari tumeshayasaini" . Amesema Ndg. Hussein
Kwa Upande wake, Meneja wa TAMESA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Bikulamchi Liberatus, amesema mambo yakienda kama yalivyokusudiwa yataleta tija kwa pande zote za Muungano kwa kubadilishana ujuzi kwa mafundi pamoja na vifaa.
Aidha Mhandisi Liberatus amesema kuwa katika makubaliano yao,fursa ya mafunzo kutoka mataifa yaliyoendelea itakapojitokeza wataungana kwa pamoja kupata ujuzi huo kwa lengo la kuleta tija kwa pande zote mbili za Muungano.
Naye,Meneja mipango TAMESA Makao Makuu Dodoma Bw. Senzo Fredrick Gwanchele ameeleza kuwa ushirikiano wao umelenga kubadilishana ujuzi kati yao kwa lengo la kuleta tija kwa kutoa huduma bora kwa wateja wao.
0 Comments