Ticker

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI HANDENI VIJIJINI YAPATA HATI SAFI, YAKUMBUSHWA KULIPA MADENI


Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni imetakiwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipia madeni yake kwa watumishi pamoja na fedha za miradi ambayo haikuendelea kutekelezwa na kukamilika kwa wakati.

Wito huo umetolewa na mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Buriani kwenye Baraza maalumu la kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), katika halmashauri hiyo ambayo imepata hati safi kwa kuongoza kujibu hoja 57 kati ya 78 zilizowasilishwa.

Dkt. Buriani kati ya hoja zilizosalia ambazo zinaendelea kupatiwa majibu, mojawapo ni ya madeni, huku akiagiza madiwani na watendaji kushirikiana na kuzifunga hoja hizo kwa haraka.

"Niwapongeze kwanza kwa kupata hati safi, ni kweli mlianza na makusanyo hafifu lakini sasa mmepiga hatua, halmashauri hii ndiyo pekee inayoongoza katika kujibu hoja, lakini niwatake kabla ya juni 30, mwaka huu hoja 21 zilizobaki zifungwe,

"Deni la sh bilioni 2.306 ni kubwa sana, nikuagize mkurugenzi wa halmashauri, utenge fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi, lakini madenu ya miradi ambayo ilichelewa kutekelezwa kwa wakati kutokana na uchelewaji wa fedha" amesema.

Sambamba na hayo, Dkt. Buriani amesisitiza pia ulipwaji wa mikopo ndani ya halmashauri kupitia fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwapa mikopo wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema halmashauri hiyo imekuwa ikisuasua katika kufuatilia ulipwaju wa mikopo hiyo kwa walengwa waliokopeshwa na kudababisha kulimbikiza madeni hivyo kuagiza ufuatiliwajh wa haraka.

"Wito wangu kwa Ofisa Ustawi wa Jamii, mikopo ambayo ina madeni iendelee kulipwa, mna deni la zaidi ya shilingi milioni 1, na hii ifanyike sambamba na ulipwaji wa madeni ya wastaafu kabla ya juni 30, mwaka huu" ameongeza Dkt. Buriani.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mussa Mwanyumbu kwa niaba ya madiwani wenzake ameahidi kizifanyia kazi na kuzifunga hoja hizi ifikapo juni 30, mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments