Ticker

6/recent/ticker-posts

INEC- ZINGATIENI WELEDI NA MAADILI YA UANDISHI WA HABARI

KATIKA kuelimisha wananchi lazima waandishi wa habari wazingatie weledi na maadili ya taaluma yao ili kuhakikisha wananchi wanashiriki mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura ambao utazinduliwa rasmi Julai, Mosi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ameyasema hayo leo Juni 14, 2024 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Mhandisi Andrew Kisaka wakati akitoa mada juu ya Wajibu na Majukumu ya Vyombo vya Habari na Utangazaji katika Kuelimisha Umma katika mkutano maalumu wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioikutanisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC,) na waandishi wa Habari.

Aidha amewataka waandishi hao kutoa taarifa kwa usahihi na kwa wakati kwa kuwa ni haki ya raia kupata taarifa mbalimbali ambazo zitawasaidi kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa maoni, kushiriki michakato mbalimbali ikiwemo ya uboreshaji wa daftari hilo.

Pamoja na hayo Mhandisi Kisaka amesema utangazaji kupitia mitandao ya kijamii nchini umekua na kufikia asilimia 33 huku mtandao wa WhatsApp ukiongoza kwa kuwa na watumiaji milioni 9.9, Facebook watumiaji milioni 8.1, Instagram watumiaji milioni 3.7,  YouTube watumiaji milioni 2.9, Tik Tok watumiaji milioni 1.6 na Mtandao wa X ( awali Twitter) ukiwa na watumiaji wapatao laki saba.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Kisheria kutoka (INEC,) Seleman Mtibora amewataka washiriki wa mkutano huo kufikisha ujumbe na kuhamasisha jamii kuhusu zoezi hilo la Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura utakaohusisha pia uandikishaji wa wapiga kura wapya.

“Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kupitia vituo 40,126 vya kujiandikisha wapiga kura kwa mwaka 2024/2025 huku vituo 39,709 vikiwa Tanzania Bara na vituo 417 vikiwa visiwani Zanzibar.” Amesema.

Post a Comment

0 Comments