Ticker

6/recent/ticker-posts

MRADI WA SLR WATENGA BILIONI 1.091 KUTEKELEZA SHUGHULI ZA MIRADI YA KIJAMII NA KIUCHUMI KWA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu, Mbeya, 25.6.2024

Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) katika mwaka 2024 umetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.091 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri saba zinazotekeleza Mradi huo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Mbeya (Jumanne Juni 25, 2024) na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa siku ya pili ya kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za mradi huo kwa mwaka 2024.

Dkt. Mapunda amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha inaweza mazingira wezeshi kwa wasimamizi wa ngazi zote za maamuzi zinazosimamia utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha fedha zilizotengewa zinawafikia kwa wakati ili kuweza utekelezaji miradi hiyo kwa wananchi.

“Katika mwaka huu wa fedha tumepanga kutekeleza jumla ya miradi sita ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi fedha zake zitaanza kutolewa na kufikishwa katika Halmashauri zote zinazotekeleza miradi…Nawasihi tuweke jicho letu katika fedha hizo ili kuhakikisha zinatekeleza malengo yaliyokusudiwa” amesema Dkt. Mapunda.

Aidha Dkt. Mapaunda ameitaja miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Malambo 3 katika Halmashauri za Wilaya za Mbarali, Wanging’ombe na Mpimbwe, Ujenzi wa Vitalu Nyumba katika Halmashauri za Wanging’ombe, Mbeya na Iringa, Ujenzi wa Kituo cha Kuchakata Maziwa katika Halmashauri za Wilaya ya Mbarali.

Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuchakata mpunga katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, ujenzi wa kituo cha kuchakata asali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na ujenzi wa kituo cha kuchakata alizeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Amefafanunua kuwa miradi hiyo imekusudia kuwawezesha wananchi kuachana na shughuli zisizo endelevu katika mazingira na hivyo kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli mbadala kwa ajili ya kujiongezea kipato katika maeneo yao.

“Mradi umepanga kuajiri Afisa Biashara ambaye kwa kushirikiana na Afisa Maendeleo ya Jamii wataweza kuwajengea uwezo wananchi kupitia vikundi vidogo vidogo ili kuendesha shughuli kwa mfumo wa kibiashara na kuuza mazao yao kwa ajili ya kujiongezea kipato” amesema Dkt. Mapunda.

Ameongeza kuwa Serikali ilianzisha mradi huo mahsusi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira ikiwamo ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji na badala yake kuanzisha shughuli mbadala kwa ajili ya kuongeza kipato kwa wananchi.

Kikao kazi hicho kinahusisha Maafisa Viungo, Maafisa Mipango,Wahandisi wa Miradi, Maafisa Manunuzi, Maafisa Misitu na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri za Wilaya zinazosimamia Mradi.

Mradi wa SLR unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 25.8 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano unaotarajia kukamilika mwaka 2025 ulioanza mwaka 2021 ukihusisha jumla ya Mikoa mitano, Halmashauri saba, Kata 18 na vijiji 54.

Halmashauri zinazonufaika na mradi huo ni Iringa Vijijini (Iringa), Wanging’ombe (Njombe), Wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR), Dkt. Damas Mapunda akizungumza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mradi huo kwa mwaka 2024 leo Jumanne Juni 25, 2024 Jijini Mbeya. Anayefuatilia mbele ni Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Thomas Chali
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kuhusu Mradi huo leo Jumanne (Juni 25, 2024) wakati wa kikao kazi hicho cha Siku tatu kinachoendelea Jijini Mbeya.

Maafisa Waandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wanaosimamia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) Bw. Julius Enock na Bi. Risper Koyi wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kuhusu Mradi huo leo Jumanne (Juni 25, 2024) wakati wa kikao kazi hicho cha Siku tatu kinachoendelea Jijini Mbeya.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kuhusu Mradi huo leo Jumanne (Juni 25, 2024) wakati wa kikao kazi hicho cha Siku tatu kinachoendelea Jijini Mbeya.

(NA MPIGAPICHA WETU)

Post a Comment

0 Comments