Ticker

6/recent/ticker-posts

SIRI YA GAWIO KUBWA TFS HII HAPA

Na Selemani Msuya

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo ametoa siri iliyosababisha washike nafasi ya tatu kwa taasisi za serikali zilizotoa gawio kubwa kwa mwaka wa fedha 2023.

Wakala huyo wa serikali jana alitangazwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kutokea kundi la taasisi zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi kwamba ametoa gawio la Sh bilioni 21.3 na kushika nafasi ya tatu, nafasi ya pili ikiwa ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa Sh bilioni 34.7 na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikishika nafasi ya kwanza iliyotoa Sh bilioni 153.9, huku TASAC ikiwa ya nne na BRELLA ya tano.

Pia ofisi hiyo Msajili wa Hazina ilitangaza Kampuni ambazo serikali ina hisa chache, ila zimetoa gawio kubwa kuwa ni NMB Sh bilioni 54.5, Twiga Mineral Corporation Sh bilioni 53.4 Airtel Tanzania Sh.bilioni 40.8, Puma Energy Sh bilioni 12.2 na RPC Moshi Sh bilioni 10.2.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii baada ya hafla ya kumkabidhi gawio Rais Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika Ikulu jijini Dae es Salaam jana, Kamishna wa Uhifadhi, Silayo amesema hawakufika hapo kwa bahati mbaya bali kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Prof Silayo amesema TFS imeweka nguvu kwenye mifumo ya ukusanyaji mapato na kufanya kazi kwenye misingi ya kijeshi, hali ambayo inaonesha kuwa kwa mwaka ujao gawio litaongezeka.

"Sisi TFS tumejipanga kuongeza gawio kutoka Sh bilioni 21.3 hadi kufikia Sh bilioni 27.2 na nguvu kubwa tunaelekeza kwenye kuimarisha na kusimamia mifumo ya ukusanyaji mapato," amesema.

Kamishna huyo amesema kwa gawio la mwaka 2023 TFS iliongeza mapato kupitia mashamba ya miti ambayo yameingiza asilimia 65 ya mapato yote, hivyo matarajio yao eneo hilo litaongeza zaidi mwaka huu wa 2024.

Prof Silayo amesema eneo lingine ambalo wanatarajia kulitumia kuongeza mapato ni ufugaji nyuki, usafishaji wa bidhaa za misitu, viwanda vya kisasa ambapo viwezesha kuongeza usafishaji wa bidhaa za misitu kwa asilimia 113.

"Mwaka huu wa 2024 hadi June hii tumeshapata zaidi ya Sh bilioni 4.6, hivyo tunaona lengo la kutoa gawio la Sh bilioni 27.2 linaenda kutimia. Ila tutaweka mkazo kwenye utalii na ufugaji, usimamizi wa mapato na kuongeza mashamba ya miti ambayo ni muhimu sana," amesema.

Amesema katika kuongeza mapato hawatarajii kuangalia eneo la mkaa kwani wanaunga mkono Kampeni ya Rais Samia ya Nishati Safi ya Kupikia.

Akizungumza wakati wa kupokea gawio Rais Samia aliipongeza TFS kwa kuongeza gawio na kuitaka isitumie mapato ya mkaa kwa ajili ya kutoa gawio kwani kwa sasa kampeni yake ni nishati safi ya kupikia, hivyo waungane naye kwa hilo. Katika hafla hiyo pia Rais Samia alitoa tuzo kwa TFS ikiwa moja taasisi zilizotoa Gawio kubwa, mchango mkubwa na kujiimarisha mwaka hadi mwaka na kutoa stahiki na kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments