Ticker

6/recent/ticker-posts

TANROADS YAMPA TANO RAIS SAMIA KUTOA BIL 101.2 KUANZA UJENZI WA KM 73 ZA LAMI BARABARA YA KAHAMA-BULYANHULU JCT – KAKOLA

Baada ya tarehe 16 Machi 2024 Serikali kusaini Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kahama-Bulyanhulu Jct - Kakola yenye urefu wa Kilomita 73 kwa kiwango cha lami, tayari Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation imeanza utekelezaji wake.

Pamoja na Barabara hiyo kufungua fursa za kiuchumi za madini, kilimo, misitu na utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma mara baada ya kukamilika pia Barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa Wasafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Tanzania kwenda nchi za jirani za Rwanda na Uganda.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Samwel Mwambungu amesema kuwa barabara hiyo inajengwa na serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 101.2 kwa ufadhili wa Kampuni ya Madini ya Barrick Tanzania Mining Companies (BTMCs).

Mhandisi Samwel ameeleza kuwa barabara hiyo itajengwa kwa muda wa Miezi 27 kwa kusimamiwa na kitengo maalumu cha ushauri wa Kihandisi ndani ya Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS (Tanroads Engineering Consulting Unit-TECU).

Amesema kuwa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu Jct – Kakola (km 73) kwa kiwango cha lami ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Mhandisi Samweli amesema kuwa kwa sasa zoezi la kuhamisha miundombinu ya mawasiliano, maji na umeme iliyopo ndani ya eneo la ujenzi vinaendelea wakati mkandarasi anaendelea na zoezi la kuleta mitambo eneo la ujenzi.

Mkandarasi amefanikiwa kupata kambi yake iliyopo kilometa 10 kutoka eneo la Manzese-Kahama na tayari ameanza zoezi la kulisafisha kwaajili ya ujenzi wa kambi hiyo.

Aidha, Mkandarasi amefanikiwa kupata sehemu ya kujenga Ofisi za Mhandisi Mshauri na tararibu za uthaminishaji wa sehemu hiyo unaendelea kwa ajili ya kuidhinisha malipo.

Post a Comment

0 Comments