Ticker

6/recent/ticker-posts

WALIOVAMIA ENEO LA NSSF KUANZA KUONDOLEWA

   

*Mkuu wa Wilaya ya Temeke afika eneo la tukio na kutoa angalizo

Na MWANDISHI WETU

Dar es Salaam. Hatimaye waliovamia ardhi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuanza kujenga makazi katika Mtaa wa Malela Kata ya Toangoma, Temeke Dar es Salaam wataanza kuondolewa rasmi katika maeneo hayo kuanzia tarehe 18 Juni 2024.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa aliyoyatoa Juni 5, mwaka huu, wakati alipofika eneo hilo na kuwakamata watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwatapeli wananchi kwa kuwauzia maeneo yanayomilikiwa kihalali na NSSF, ambapo aliagiza wavamizi wote wa ardhi kuondolewa.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda tarehe 15 Juni 2024 amefika eneo hilo kuendelea kutilia msisitizo wa namna ambavyo NSSF itatekeleza maelekezo yake ya kuwaondoa waliovamia maeneo ya miundo mbinu ya barabara na maji.

Mhe. Mapunda amesema eneo la Malela historia inaonesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2002 Serikali ilichukua eneo hilo kupitia Wizara ya Ardhi na ikawalipa fidia wakazi wote wa asili na kuwa mwaka 2005 mpaka 2008 Wizara ya Ardhi ilikuwa inayagawa kwa kuyauza maeneo hayo kwa watu binafsi na Mashirika ikiwemo NSSF ambayo iliuziwa eneo hilo na walipewa hatimiliki.

Amebainisha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2017 kwa nyakati tofauti, wananchi walianza kuvamia eneo hilo na kuwa kati ya mwaka 2020 na 2022 uliitishwa mkutano wa wavamizi baina ya NSSF na uongozi wa Serikali ambapo katika kueleweshana ikaonekana si busara waliovamia kipindi hicho kuondolewa hivyo wakakubaliana kuwa waliovamia waingizwe kwenye mpango wa matumizi ya ardhi na NSSF.

"Baada ya hapo yakawekwa makubaliano kuwa walioingizwa kwenye mpango na NSSF washirikiane na Mfuko wasiwepo watu wengine watakaovamia, lakini kilichotokea kati ya mwaka 2002, 2003 na 2004 waliovamia walikuwa wengi kuliko wale waliokuwepo mwanzoni," amesema Mhe. Mapunda.

Amesisitiza kuwa, waliokuwepo kwenye mpango wa matumizi ya ardhi ambao ni takribani 145 walishaongea na NSSF na tayari walishakubaliana.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja Milki wa NSSF, Bw. Geofrey Timoth amesema katika kutekeleza maelekezo hayo ya  Waziri wa Ardhi, NSSF inatarajia kuondoa nyumba zote ambazo zipo kwenye barabara na miundo mbinu ya maji pamoja na kuhakiki watu wachache ambao wanadai walikuwepo tokea mwaka 2021/22.

Bw. Timoth amesema zoezi hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliyotoa wiki iliyopita.

Amebainisha namna ambavyo NSSF wanaenda kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Ardhi ni kuwa bàadhi ya maendelezo yaliyofanywa ambayo waliyabaini mwaka 2021 na 2022 wamekubaliana kuwa watakaa na wahusika kwa sababu yapo kwenye mpango wa ardhi.

"Kwa hiyo tutakaa na wahusika na tutawaambia ni nini cha kufanya ili waendelee kuwa na amani kwenye maeneo husika," amebainisha Timoth.

Ameendelea kubainisha kuwa maeneo ambayo yaliendelezwa nje ya mwaka 2021/22 yataenda kuondolewa kwa sababu NSSF ina mpango wa kuyaendeleza pamoja na utaratibu wa kuzuia uvamizi kwenye maeneo mengine.

Post a Comment

0 Comments