Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MELI kubwa iliyobeba mizigo ya tani elfu 14 imetia nanga katika bandari ya Tanga kutoka nchini China kwa mara ya kwanza baada ya uboreshwaji mkubwa wa bandari hiyo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 429.
Meli hiyo ya kampuni ya Seefront Shipping Service Ltd, imebeba magari 500 ya mizigo ambayo yanasafirishwa kwenda nchi za DRC Congo, Zambia, Burundi na Rwanda unatarajiwa kukaa bandarini hapo kwa muda wa siku tatu na kuondoka.
Akishuhudia mapokezi ya meli hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema fedha zilizowekezwa katika maboresho hayo zimeanza kuonesha mafanikio kwani utendaji kazi katika bandari hiyo umekuwa wa tija.
"Shughuli hii ya leo maana yake ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa maboresho, shehena zimeongezeka mara dufu kutoka shehena 470 mwaka 2019 na kufikia milioni 1 ya sasa, lakini pia meli zimeongezeka kutoka 118 mwaka 2019 hadi 307 mwaka huu,
"Haya ni mapinduzi makubwa yanayoonesha kwamba fedha zilizowekezwa zinaleta tija, hongereni kwa usimamizi mzuri, wastani wa kuongeza uhudumiaji wa meli kila mwaka unadhihirisha fedha iliyowekezwa hapa haikutupwa, lakini pia watendaji hawa kulala usingizi" amesema.
Pamoja na hayo kwa upande wa makasha na abiria wameongezeka lakini pia hata mzunguuko wa fedha kwa Mkoa umeongezeka, hivyo kukamilisha maana ya kauli mbiu ya Mkoa huo kwamba 'Tanga lango kuu la uchumi Afrika'.
Hata hivyo Naibu Kihenzile alitoa rai kwa Mamlaka ya Bandari nchini kuendelea kuisimamia bandari ya Tanga kwa weledi lakini pia kwa wadau kuchangamkia fursa za kusafirisha abiria kutoka bandarini hapo kwenda visiwa vya Pemba.
"Naumia nafasi hii kuwaomba wadau, ukiangalia idadi ya abiria haiongezeki kwa kasi lakini hapa tunayo fursa ya kuwatoza abiria Pemba na Unguja na kuealeta hapa Tanga, meli hazitoshi njooni leteni meli hapa" amesisitiza Kihenzile.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema Mkoa upo kimkakati ambao una uwezo kibiashara na maboresho hayo yatapunguza wigo wa wafanyabiashara kurundika mizigo bandari ya Dar es salaam kwa kuipitishia Tanga.
"Ukitumia bandari ya Tanga, kwanza mizigo yako itatoka kwa haraka, hakuna usumbufu wa kusubiria meli nyingine ipakue, wenye mizigo mikubwa watakaa siku tatu na kwa wale wenye mizigo midogo huchukua siku moja, na hilo tunawahakikishia wateja wetu"
"Niwaombe wadau wote wenye makampuni ya wakala wa meli waendelee kutumia bandari yetu ya Tanga na ujio wa meli hii kutia nanga hapa ni faraja kubwa kwa Mkoa wetu na ni imani yetu kuwa uwepo wa meli hii unaendelea kupanua wigo na fursa za kibiashara,
Pamoja na hilo, itasaidia kupunguza garama za usafirishaji, lakini vilevile unaendelea kurahisisha biashara na kupunguza muda wa bidhaa kuwasili katika maeneo yetu" amebainisha Dkt. Buriani.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema kupitia maboresho hayo tayari wameshaingiza meli kubwa zipatazo 35 zilizobeba tani laki 330,173, "kwa mwezi huu wa saba tulioanza mwaka mpya 2024/25 tumesha pokea meli 31, wakati tulijiwekea lengo la kupokea meli 19, tumevuka lengo kabla mwezi haujakwisha,
"Tunaona mwanzo mzuri, mwaka Jana mwezi kama huu tulihufumis meli zenye tani elfu 46 na mwaka huu kabla mwezi haijaisha tumehudumis tani elfu 96, kwahiyo hii ni dalili njema na mwaka huu tumewekewa lengo la tani milioni 1.4" amesema Mrisha.
0 Comments