Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA wa Urais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Emmanuel Muga, amesema hakuna uoenevu kwenye uchaguzi wa Urais ndani ya chama hichovkama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Muga alitoa kauli hiyo kwenye mdahalo wagombea wa kinyang'anyiro hicho ulioendeshwa na kituo cha Televisheni cha Star Tv na kushirikisha wagomnea wote sita.
Alikuwa akijibu swali lililoulizwa na mwananchi kuhusu kuenguliwa kwa mgombea mwenzake Boniface Mwabukusi na kisha kurejeshwa tena kwa amri ya mahakama.
Muga alisema si vyema kuhusisha siasa katika uchaguzi huo na kukuza mambo ambayo hayapo kwenye mchakato wake na kwamba yeye anaamini unaendeshwa kwa haki tofauti na inavyotaka kuaminishwa kwenye jamii.
alisema ni vema watu kuacha kuchanganya siasa na uchaguzi huo kwa kuwa unafanyika kitaaluma bila uonevu.
“Mimi nadhani kwamba tuache siasa na mambo ya dhana kwa sababu sisi ni wanasheria, ndani ya TLS hakuna uonevu, naomba muelewe kitu kimoja, kuna kamati ambazo tumeziunda sisi wenyewe, na hii kamati iliyomwengua Mwabukusi, ni kamati ambayo imeundwa na mawakili na siyo mtu mwingine ametoka nje.Sisi tunaoenda mahakamani, huwa tunakutana mara nyingi na maamuzi kama haya,"alisema Muga.
“Lakini ukishakumbana na maamuzi kama hayo, hugeuki ukashika kichwa ukaanza kupiga mateke kwenye mchanga unalalamika,hapana, unafanya uamuzi wa kwenda juu, ukiamini kwamba kile ambacho nimenyimwa huku chini, bila shaka juu nitakipata, kwa hiyo ni aina ya mfumo wa utoaji haki."
“Kwenye kamati ya uchaguzi ya TLS, Mwabukusi alipata haki, akaruhusiwa kugombea, lakini kamati ya rufani ambayo inaundwa na mawakili ikamwengua, lakini mahakama Kuu ikamrudisha, kwa hiyo ni mfumo ambao tumeuozoea sisi, lakini ilivyopokelewa nje, ilivyoelezwa, utafikiri sisi siyo wanasheria. Tusikuze jambo,”alisema Muga.
Mbali na Muga, wagombea wengine katika nafasi hiyo ya Urais TLS ni Sweetbert Nkuba, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, Kapteni Ibrahimu Bendera na Boniface Mwabukusi.
0 Comments