-Wawekezaji kwenye viwanda vya kuongeza thamani madini mkakati wakaribishwa.
-Mpango wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wajadiliwa
Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde leo Jijini Dar es salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe maalum kutoka Serikali ya Indonesia uliiongozwa na Mhe. Pahala Nugraha Mansury, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.
Akieleza kuhusu mikakati ya sekta, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Tanzania ni moja ya Nchi zilizobarikiwa madini aina zote yakiwemo madini mkakati ambayo Serikali imeweka utaratibu mahsusi kwa mwekezaji yeyote katika eneo hilo.
"Kwa upande wa madini mkakati, nchi yetu tumeweka utaratibu wa wazi kabisa kwamba, mwekezaji yeyote atayekuja kuwekeza katika madini mkakati ni lazima ayaongeze thamani hapa hapa nchini, hivyo nawakaribisha sana Indonesia kuwekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani madini" amesema Mavunde.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina wa High Resolution Airborne Geophysical Survey kuwa zaidi ya asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, na kutumia fursa hiyo kualika wadau mbalimbali kutoka Indonesia kuja kuunga mkono mpango huo na husasan katika kuwajengea uzoefu wataalamu wa Tanzania.
"Tanzania ni kati ya Nchi chache Afrika zilizoweka utaratibu mzuri wa kusimamia wachimbaji wadogo chini ya ulezi wa STAMICO.Wachimbaji hawa wadogo wamekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Nchi, na kutoa rai kwa Indonesia kuja na mpango wa kubadilishana uzoefu ili kuwaendeleza zaidi wachimbaji wadogo," amesisitiza Waziri Mavunde.
Akieleza kuhusu lengo la ujio wao, Naibu Waziri Mansury amesema kubwa ni kuimarisha ushirikiano wa Indonesia na Tanzania kwakuwa nchi hizo ni marafiki na hilo linashuhudiwa na ziara kubwa mbili za viongozi wakuu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu na Mhe. Rais Joko Widodo kutembeleana kwa lengo la kuimarisha mahusiano katika sekta mbalimbali hususan katika sekta ya madini na kuongeza kuwa Indonesia ina lengo la kuwa kitovu cha uzalishaji wa betri za gari za umeme, hivyo wanaiona fursa kubwa kwa mshirika wake Tanzania hususan katika madini mkakati ya graphite, nikeli, shaba na lithium.
Aidha, Naibu Waziri Mansury amepongeza jitihada za Tanzania kwenye utafiti kupitia Vision 2030 na kuahidi kwamba Serikali ya Indonesia ipo tayari kushirikiana zaidi ili kutimiza maono hayo ya kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina wa kurusha ndege.
0 Comments