MENEJA wa Kanda ya kati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Bi.Hawa Lweno,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la EWURA katika maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati imewataka wananchi kutumia maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao, kuwekeza kwenye vituo vya mafuta vya gharama nafuu maeneo ya vijijini na mafundi umeme kupata utaratibu wa kuomba leseni EWURA.
Akizungumza Meneja wa Kanda ya kati wa Mamlaka hiyo, Bi.Hawa Lweno,amesema maonesho hayo ni eneo muhimu ambalo wananchi wanaweza kupata elimu kuhusu shughuli za udhibiti hivyo anawakarinisha kutembelea banda la EWURA.
“Moja kati ya majukumu yetu ni kuhakikisha kuwa tunatatua migogoro baina ya watumiaji huduma pamoja na watoaji huduma, kutoa leseni na vibali mbalimbali hivyo katika kipindi hiki cha maonesho tunatoa wito kwa wananchi waje kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali” amesema Bi.Hawa
Aidha,amewataka wananchi kujenga tabia ya kutembelea ofisi au kuingia kwenye tovuti za watoa huduma wanaodhibitiwa na EWURA kama mamlaka za maji na TANESCO ili wapate mikataba ya huduma kwa wateja itakayo wasaidia kujua haki na wajibu wao katika kupokea huduma hizo.
Aidha amesisitiza kuwa, EWURA inao utaratibu mzuri wa kutoa leseni kwa mafundi umeme wote nchini kupitia mfumo wa kieletroni wa LOIS unaopatikana katika tovuti ya Mamlaka hiyo www.ewura.go.tz, ambao fundi umeme anaweza kuutumia kutuma maombi popote alipo.
Kwa upande wa vituo vya mafuta maeneo ya vijini, Meneja huyo ameeleza kuwa EWURA imerahisisha masharti ya uwekezaji ili kushamirisha huduma na kupiga vita uuzaji holela wa bidhaa za petroli katika maeneo yasiyo na vituo vya mafuta vya kutosheleza mahitaji.
WANANCHI mbalimbali wakiwa katika banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati wakipata elimu kuhusu haki na wajibu wao katika maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma
0 Comments