WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na Serikali ya Cuba kujenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha chanjo mbalimbali ikiwemo chanjo ya homa ya ini.
Amesema viwanda vya dawa nchini Cuba vikiwemo vinavyotengeneza dawa zinazotokana na mimea tiba vimeiwezesha nchi hiyo kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje ya nchi hiyo kwa asilimia 60 .
Ameyasema hayo Agosti 13, 2024 alipotembelea kiwanda na kituo cha Utafiti cha LABIOFAM kilichopo nchini Cuba ambacho kinazalisha bidhaa mbalimbali za binadamu, kilimo na mifugo. Waziri Mkuu alikuwa nchini Cuba katika ziara maalumu ya kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Alisema kiwanda hicho kinashirikiana na kiwanda cha Viuadudu cha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) cha LABIOFAM kilichopo Kibaha mkoani Pwani ambacho kinatengeneza viuadudu vitakavyopulizwa kwenye mazalia ya mbu nchini kote na Afrika ili kuangamiza mbu na kutokomeza ugonjwa wa maralia.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Afya ishirikiane na Ubalozi wa Tanzania uliopo Havana nchini Cuba kuandaa ziara itakayowezesha kufanyika mazungumzo na Wizara ya Afya ya Cuba, viwanda, taasisi na mashirika yanayotengeneza dawa mbalimbali nchini humo.
Mheshimiwa Majaliwa alisema lengo la mazungumzo hayo ni kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha dawa hizo kuuzwa nchini baada ya kupata vibali kutoka vyombo na taasisi zenye dhamana ya kuidhinisha matumizi ya dawa nchini.
Mheshimiwa Majaliwa alizitaja dawa hizo kuwa ni pamoja na dawa za kutibu maumivu ya viungo (Rheumatoid Arthititis) na dawa ya kutibu vidonda kwenye miguu kwa watu wanaokuwa na ugonjwa wa kisukari.
Waziri Mkuu alisema kiwanda cha Labiofam kinazalisha bidhaa mbalimbali za binadamu, kilimo na mifugo ambazo kutokana na ubora na umuhimu wake zinatumika katika nchi mbalimbali.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda kingine kikubwa na Kituo cha Utafiti cha CIGB kinachotengeneza bidhaa mbalimbali za afya na tiba.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Majaliwa aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Balozi Hamphrey Polepole.
0 Comments